Tanzania inatarajia kuweka historia mpya kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Doha Dialogue kuhusu uhamaji wa nguvu kazi na ajira, utakaofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 6 Oktoba 2026 katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Mkutano huu wa kiwango cha juu kimataifa unatazamiwa kuwakutanisha wajumbe na viongozi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Baraza la Ushirikiano wa nchi za Ghuba ambazo ni Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain, pamoja na Jordan na Lebanon (GCC+), huku ukiwa na lengo kuu la kuimarisha ushirikiano katika kusimamia uhamaji wa nguvu kazi na kukuza ajira zenye staha.
Mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumzia maandalizi na umuhimu wa mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Clement Sangu, amesema kuwa mkutano huo unakuja kufuatia mafanikio ya mkutano wa kwanza uliofanyika jijini Doha, Qatar, tarehe 21 hadi 22 Mei 2024, ukihusisha nchi 33 zikiwemo nchi 25 za Afrika na nchi za Ghuba pamoja na Jordan na Lebanon.
Katika mkutano huo wa kwanza, Tanzania ilishiriki kikamilifu kupitia ujumbe ulioongozwa na Wizara yenye dhamana ya Kazi na Ajira, ambapo Doha Declaration iliweka msingi thabiti wa kuendeleza majadiliano na ushirikiano huo kila baada ya miaka miwili.
Waziri Sangu amefafanua kuwa maeneo muhimu yatakayojadiliwa katika mkutano huu wa Dar es Salaam ni pamoja na uimarishaji wa mikataba ya ajira baina ya nchi na nchi (Bilateral Labour Migration Agreements), uoanishaji wa ujuzi wa wafanyakazi na mahitaji halisi ya soko la ajira, na ujenzi wa mifumo ya uhamaji wa nguvu kazi inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji mapya ya soko la ajira lenye staha.
Aidha, mkutano huo utatoa fursa ya kimkakati kwa Tanzania kuimarisha nafasi yake katika mijadala ya kimataifa kuhusu uhamaji wa nguvu kazi, kupanua fursa za ajira nje ya nchi, kulinda haki za wafanyakazi wahamaji, na kuongeza ushindani wa nguvu kazi ya Kitanzania huku ukichangia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeelezwa kuendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uhamaji salama na wenye tija kwa wafanyakazi wahamaji kupitia mikataba ya kimataifa na nchi za Ghuba, kuunganisha wafanyakazi wahamaji na fursa za ajira katika nyanja mbalimbali kama vile kilimo, mifugo, utabibu, ujenzi, uhandisi, udereva, upishi na huduma za majumbani.
Hatua nyingine ni pamoja na kuweka utaratibu wa kusajili na kusimamia wakala binafsi wa ajira kwa kuzingatia sheria na viwango vya kimataifa, kuweka mifumo ya kuwezesha rasilimali fedha kwa wafanyakazi kugharamia mahitaji muhimu, na kuimarisha mifumo ya kidijitali ikiwemo Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Soko la Ajira unaolenga kuboresha uajiri na ulinzi wa wafanyakazi wahamaji.
Waziri Sangu amesisitiza kuwa Mkutano wa Pili wa Doha Dialogue ni fursa ya kipekee ya kugeuza ahadi na makubaliano kuwa hatua za vitendo na matokeo yanayopimika, akibainisha kuwa Tanzania inaamini kupitia ushirikiano thabiti kati ya Afrika na GCC+, mkutano huo utaimarisha uhamaji salama, rasmi, wa haki na endelevu, kufungua milango ya ajira kimataifa kwa Watanzania, na kujenga misingi ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi zinazopeleka na zinazopokea wafanyakazi.
Mkutano huo unafanyika huku idadi ya watanzania wlaiopo nchi za nje kwa kupitia mifumo ya serikali wanakadiriwa kufikia elfu 15 kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu na kwamba mipango zaidi ikiwa inasukwa ya ajira zaidi.
Katika kikao hicho na waandishi wa habari Waziri Sangu pia amesema kwamba hivi karibuni watatangaza ajira 600 za wahandisi na mafunbdi mchundo.
Aidha alisema kwamba traifa linazidi kupata heshima kutokana na nguvu kazi inayoenda nje kujua wajibu wake kujituma na kuwa na nidhamu. Anasema hayo ni matokeo ya utaratibu mzima wa kuweka mazingira sawa na kuwezesha watanzania kutafuta kazi zenye staha ughaibuni.
