` SUNGURA AHIMIZA UADILIFU WA TAARIFA NA UPATIKANAJI WAKE

WANDAMAN HOTEL

SUNGURA AHIMIZA UADILIFU WA TAARIFA NA UPATIKANAJI WAKE


Na Beda Msimbe, BSKY Media
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mwenyekiti wa Muungano wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI),Ernest Sungura amesema katika zama za sasa changamoto kuu si uhaba wa taarifa bali ni mafuriko ya taarifa potofu zinazosambazwa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii na teknolojia ya Akili unde.
Aidha amesema kwamba upatikanaji wa taarifa pekee hautoshi, bali wananchi wanahitaji taarifa sahihi, zinazopatikana kwa wakati na zinazoaminika ili kuweza kufanya maamuzi sahihi na kushiriki kikamilifu katika masuala ya umma.

Sungura alisema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa Duniani yaliyofanyika Septemba 28, 2026 jijini Dar es salaam.

Aidha, katika hotuba yake ya ufunguzi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika hoteli ya Protea alionya kuhusu ombwe la taarifa linalotokana na taasisi za umma kuchelewa au kushindwa kutoa taarifa rasmi mara nyingi na kutoa mwanya kwa wananchi kujazwa na uvumi na upotoshaji.
Anasema ili kukabiliana na hili, taasisi za umma zinatakiwa kuimarisha utamaduni wa kutoa taarifa kwa hiari na mapema bila kusubiri kuombwa, huku vyombo vya habari na wanahabari wakikumbushwa wajibu wao wa kuthibitisha ukweli badala ya kukimbilia kasi.

Mkutano huo ulitumia mifano mbalimbali ya kihistoria na ya hivi karibuni ndani na nje ya nchi kuonyesha kuwa kuficha au kuadhibu vyombo vya habari hakuzuii ukweli kujitokeza, bali kunaondoa imani ya wananchi kwa taasisi za umma.

Katika maadhimisho hayo wadau walitaka kuwapo kwa ushirikiano katika kujenga uelewa wa umma, kuimarisha sheria za upatikanaji wa taarifa, na kuhamasisha matumizi ya ustadi wa kuchuja na kuthibitisha taarifa.

Aidha badala ya kulalamika kuhusu ukosefu wa taarifa, wadau walihimizwa kushirikiana ili kuhakikisha habari za kuaminika zinawafikia wananchi kwa wakati muafaka, huku wakisisitiza kuwa uadilifu wa taarifa ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa dhati kutoka serikalini, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wananchi wenyewe.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464