` SERIKALI YAFANYA KIKAO KAZI CHA KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NINO

WANDAMAN HOTEL

SERIKALI YAFANYA KIKAO KAZI CHA KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NINO

  

Ofisa kutoka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Bw: Mosses Chilla, akifungua kikao cha wataalamu wa ngazi ya Mkoa kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Baadhi ya wataalamu wa kamati za maafa za Mkoa wa Dar es Salaam.

DAR ES SALAAM, 28 SEPTEMBA 2026 — Serikali imeanza maandalizi ya kina ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazotarajiwa kunyesha za EL Nino katika msimu wa Oktoba 2026, kwa kuendesha kikao kazi pamoja na ziara za ufuatiliaji katika mikoa yote nchini  nzima ili kutathmini utayari wa mamlaka za mikoa na wilaya.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mifumo ya usimamizi na uratibu wa maafa inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa na elimu sahihi kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa kabla, wakati na baada ya mvua hizo.

Katika ziara hizo, Serikali itafuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi za mikoa na wilaya, huku viongozi wa maeneo husika wakitakiwa kuimarisha maandalizi na mifumo ya mwitikio wa haraka endapo kutatokea mafuriko, uharibifu wa miundombinu au majanga mengine yanayohusiana na mvua.

MIUNDOMBINU NA BARABARA

Miongoni mwa maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni ukaguzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na mifereji ya maji, pamoja na kuhakikisha mifereji inasafishwa ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kupunguza uwezekano wa mafuriko katika maeneo ya makazi na biashara.

Aidha, utayari wa mitambo na vifaa vya dharura vinavyomilikiwa na TANROADS na TARURA utafuatiliwa ili kuhakikisha vinapatikana na vinaweza kutumika kwa wakati kurejesha mawasiliano endapo barabara au madaraja yataharibika.

AFYA NA USALAMA WA MAJI

Katika sekta ya afya, Serikali itahakiki utayari wa vituo vya afya, ikiwemo upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na mahitaji muhimu ya kukabiliana na magonjwa yanayoweza kuongezeka wakati wa mvua na mafuriko.

Mamlaka husika pia zitatakiwa kuimarisha hatua za kuhakikisha usalama wa maji ya matumizi ya wananchi, pamoja na kutoa elimu kuhusu usafi wa mazingira na matumizi salama ya maji ili kupunguza hatari ya milipuko ya magonjwa yanayoweza kuhusishwa na uchafuzi wa maji.

MAENEO SALAMA NA ZANA ZA UOKOAJI

Serikali pia itafuatilia utambuzi na maandalizi ya maeneo salama kwa ajili ya kuwahifadhi wananchi ambao wanaweza kuathiriwa na mafuriko au majanga mengine yatayotokana na mvua hizo.

Vilevile, utayari wa zana na vifaa vya uokoaji vitakavyotumika wakati wa dharura, ikiwemo vile vinavyosimamiwa na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, utakaguliwa ili kuhakikisha mwitikio wa uokoaji unafanyika kwa wakati.

USALAMA WA CHAKULA NA MIFUGO

Katika sekta ya kilimo na mifugo, mamlaka za maeneo zitatakiwa kuwahimiza wakulima kuchukua hatua stahiki kulingana na ushauri wa wataalamu, ikiwemo kuvuna mazao yaliyokomaa mapema pale inapofaa na kuhifadhi mazao katika maeneo salama.

Kwa upande wa mifugo, wananchi wanaofuga katika maeneo hatarishi, hususan mabondeni, wanahimizwa kuchukua hatua za mapema za kuhamisha mifugo kwenda maeneo salama ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko.

ELIMU KWA UMMA

Serikali imeelekeza pia kuimarishwa kwa utoaji wa taarifa na elimu kwa umma kuhusu tahadhari za kuchukua kabla na wakati wa mvua, ikiwemo kuepuka kuvuka mito au maeneo yenye maji mengi, kutokujenga katika maeneo hatarishi na kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.

Hatua hizo ni sehemu ya maandalizi ya Serikali ya kuimarisha uwezo wa taifa wa kukabiliana na majanga na kupunguza madhara kwa maisha ya watu, mali na miundombinu endapo mvua kubwa au mafuriko yatatokea.

Serikali imewahimiza viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri na wananchi kwa ujumla kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua hatua za tahadhari kwa wakati.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464