` OTHMAN MASOUD OTHMAN AAHIDI KUSIMAMIA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA KWA MASLAHI YA WAZANZIBARI

WANDAMAN HOTEL

OTHMAN MASOUD OTHMAN AAHIDI KUSIMAMIA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA KWA MASLAHI YA WAZANZIBARI


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameanza rasmi majukumu yake kwa kuweka wazi azma yake ya kusimamia Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa lengo la kuimarisha mshikamano, umoja, na usawa miongoni mwa wananchi.
Akizungumza katika hafla ya kumpokea huko Pemba ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuapishwa kushika wadhifa huo, Othman alisisitiza kuwa chama chake hakikuingia katika serikali hiyo kwa ajili ya kugawana vyeo, bali kimechukulia nafasi hiyo kama dhamana ya kushirikiana kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la wananchi wote wa Zanzibar.

Aliongeza kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa si uwanja wa kushindana kisiasa bali ni mahali pa kushirikiana, akionya kuwa yeyote anayechukulia nafasi hiyo kama safari yake binafsi atashangazwa na mwelekeo huo kwa sababu nia kuu ni kusafiri pamoja kwa ajili ya manufaa ya umma.

Katika kuelezea vipaumbele vyake vya uongozi, Othman alibainisha kuwa miongoni mwa mambo ya msingi watakayoyasimamia kwa dhati ni pamoja na upatikanaji wa katiba mpya, sheria mpya, mfumo mpya wa chombo cha kusimamia uchaguzi, utumishi wa umma ulionyooka, na uimarishwaji wa vyombo vya haki vitakavyomwezesha kila mwananchi kupata haki yake bila upendeleo. Akitoa mifano ya kimataifa, alitaja nchi za Singapore na Malaysia ambazo zilikabiliwa na changamoto za migogoro lakini zikafanikiwa kujiletea maendeleo makubwa kwa kujenga taifa lenye mshikamano kupitia dhana ya umoja.

Alisisitiza kuwa kauli mbiu ya "Zanzibar Moja" si maneno ya kisiasa au propaganda ya wakati wa kampeni, bali ni msisimko thabiti utakaosimamiwa hadi dakika ya mwisho ili kujenga jamii inayopendana na kuheshimiana, ambapo hakuna Mzanzibar atakayekuwa juu ya mwingine kwa sababu ya nasaba au itikadi ya chama cha siasa.

Aidha, Othman alifafanua kuwa uwepo wa ACT Wazalendo ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa hautazuia chama hicho kutekeleza majukumu yake ya kisiasa ya kuhoji na kusukuma mambo yaende vizuri.

Alieleza kuwa ushirikiano huo kati yao na Chama Cha Mapinduzi (CCM) utaendelea kuimarisha uwajibikaji kupitia usimamizi na ufuatiliaji wa karibu wa utendaji wa serikali, huku lengo kuu likiwa ni kulinda na kutetea maslahi mapana ya wananchi wa Zanzibar.




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464