Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa 2026/2027 hadi 2030/2031 umesema kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kuimarisha hadhi yake kidiplomasia na kiuchumi katika jukwaa la kimataifa kupitia utumiaji mzuri wa rasilimali za kijiografia na kiutamaduni ili kujenga uchumi imara na stahimilivu.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kuwa utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024, hususan kupitia diplomasia ya uchumi, umefanikiwa kuratibu upatikanaji wa fursa mbalimbali za uwekezaji, masomo, masoko ya bidhaa, utalii, uchumi wa buluu, ajira kwa Watanzania, na upatikanaji wa mikopo na misaada yenye masharti nafuu.Akifafanua kuhusu mkakati huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alieleza kuwa utekelezaji wa diplomasia hiyo ulihusisha pia masuala yasiyo ya kijadi kama vile siasa, ulinzi na usalama ili kufikia malengo mapana ya maendeleo ya taifa.
Katika kipindi kilichopita, mpango huo ulibainisha kuwa Tanzania ilishiriki mikutano 43 ya Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano na mashauriano ya kisiasa, sambamba na kufanya ziara 90 za viongozi wakuu wa kitaifa nje ya nchi na kupokea ziara 33 za viongozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa nchini.
Jitihada hizi zimeleta mafanikio makubwa yakiwemo upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo, vibali vya safari za moja kwa moja za mashirika ya ndege, na kuimarika kwa mchango wa Watanzania waishio nje ya nchi katika sekta za fedha, nyumba, kilimo na viwanda.
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2024, shughuli za uchimbaji madini ziliongoza kwa kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 442.2, zikifuatiwa na sekta ya fedha na bima, uzalishaji viwandani, na sekta ya habari na mawasiliano, huku uwekezaji katika sekta za kilimo, ujenzi na usafirishaji ukiongezeka kutoka asilimia 5.8 mwaka 2023 hadi asilimia 19.4 mwaka 2024.
Ili kuendeleza kasi hiyo, Mpango wa Nne wa Maendeleo umeweka malengo mahususi ya kufikisha hisa za uwekezaji binafsi wa nje kufikia Dola za Marekani milioni 38,588 na uwekezaji wa nje kufikia Dola za Marekani milioni 659 ifikapo mwaka 2030/2031, huku hisa za uwekezaji binafsi wa nje wa moja kwa moja zikilengwa kufika Dola za Marekani milioni 28,752.53.
Wizara imesema mabadiliko ya siasa za duniani yameifanya Tanzania kuongeza juhudi za kujipambanua kama mshirika wa kuaminika katika nishati mbadala, usalama wa chakula, na uchumi wa kidijiti, huku ikihimiza uwekezaji katika bandari za kisasa, akili bandia, na mifumo ya kidijiti ili kuongeza ushindani wa kitaifa.
Ushirikiano wa karibu na jumuiya za kikanda na kimataifa kama vile EAC, SADC, AU, AfCFTA na nyinginezo umezidi kuimarisha amani, biashara, na ushawishi wa nchi, huku miradi ya kimkakati kama vile mji wa kiuchumi na bandari ya Bagamoyo ikitarajiwa kuendelea kuinua hadhi ya Tanzania kuwa kitovu kikuu cha biashara na uchumi wa buluu duniani.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464