` BANDORA ACHANGIA MIFUKO 20 SHULE YA MAPINDUZI *B" HUKU AKIWAASA WAHITIMU KUMTEGEMEA MUNGU

WANDAMAN HOTEL

BANDORA ACHANGIA MIFUKO 20 SHULE YA MAPINDUZI *B" HUKU AKIWAASA WAHITIMU KUMTEGEMEA MUNGU

 


Na Suzy Butondo Shinyanga 

Mgeni rasmi katika mahafali ya 21 ya darasa la Saba Shule ya Msingi Mapinduzi "B" manispaa ya Shinyanga Salum Bandora, amewataka wanafunzi wanaohitimu masomo yao kuendelea kumtumaini Mungu, kuishi kwa maadili mema na kuwa na hofu ya Mungu ili wasishawishike kujiunga na makundi yenye tabia na mienendo isiyofaa huku alichangia mifuko 20 ya saruji


Bandora ambaye ni diwani wa kata ya Chemchem wilayani Tabora ametoa kauli hiyo  katika mahafali yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Mapinduzi "B"iliyopo Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga, akiwataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kwa kujenga maisha yao na jamii kwa ujumla.

Amesema baada ya kumaliza shule watoto wanakutana na changamoto na vishawishi mbalimbali, hivyo ni muhimu kumtegemea Mungu, kusimamia maadili mema na kufanya maamuzi yanayowalinda dhidi ya makundi yasiyofaa.

“Nawaomba sana wanangu, mnapoendelea kusubiri matokeo yenu, msijiingize kwenye makundi yasiyo na maadili mema, ikiwemo makundi ya wavuta bangi na vijana wanaojihusisha na vitendo visivyofaa. Kaeni kwa heshima na waheshimuni wazazi wenu,” amesema Bandora.

Ameongeza kuwa wahitimu wanapaswa kumshika Mungu katika maisha yao ya kila siku na kujiuliza kabla ya kufanya jambo kama linampendeza Mungu au la.

“Msimuache Mungu. Mkitenda mema mtakuwa viongozi bora na viongozi imara hapo baadaye,kwani  maisha yenu ya baadaye yanategemea maamuzi mnayofanya leo, hivyo chagueni marafiki wanaowajenga na si wanaowapeleka kwenye uovu,” amesema.

Bandora ambaye pia ni mlezi wa Shule ya Msingi Mapinduzi B na Katibu wa Elimu Malezi na mazingira wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga, ametoa mchango wa mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya kukarabati maeneno mbalimbali  ya shule hiyo, ambapo pia aliambatana na mdau wa elimu Christian Msipi ambaye naye alichangia mifuko 10 ya saruji huku viongozi na wageni waalikwa wakichangia na kufikia mifuko 60.

Aidha amempongeza mwalimu Mkuu wa shule hiyo kwa kushirikiana na walimu wenzake na kuleta mabadiliko ya ufaulu mzuri kwa muda mfupi katika shule hiyo, amesma ni mwalimu bora na amemtaka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha shule hiyo inazidi kufanya vizuri.

“Yale ambayo yanatakiwa kutatuliwa nitayafikisha sehemu husika ili yaweze kutatuliwa kwa wakati. Pia nitamfikishia Meya wa Manispaa hii Salum Kitumbo ili kwa kushirikiana na Diwani wa Kata hii kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa,” amesema Bandora.

Kwa upande mwingine, Bandora amewaomba wageni waalikwa pamoja na wazazi kushirikiana katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo kwa kuchangia kile walichonacho kwa moyo wa upendo.

“Mimi kama mgeni rasmi naomba mniunge mkono, wageni waalikwa na wazazi, kwa kuchangia tulichonacho kwa moyo wa upendo kwa ajili ya kufanya ukarabati wa shule yetu. Mimi nitachangia mifuko 20 ya saruji na tripu moja ya mchanga, leo nitakabidhi fedha za kununua mifuko 10 ya saruji,” amesema.

Pia amewataka wananchi kuendelea kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na mifereji ya maji inapitisha maji vizuri ili kupunguza athari za mvua.

Amesema pia ni muhimu wananchi kuendelea kuwaombea viongozi wa Taifa, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Msipi ambaye ni mdau wa elimu pia ameomba orodha ya majina ya wanafunzi wote wanaotoka katika familia zenye uhitaji, akiahidi kugharamia vifaa vyao vya shule kwa ajili ya kuanzia  kidato cha kwanza.

Mbali na hilo, ametoa shilingi 2,000 kwa kila mwanafunzi aliyehitimu, pamoja na kuchangia mifuko 10 ya saruji kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo.

Katika risala ya Shule ya Msingi Mapinduzi B imeeleza kuwa inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji ushirikiano wa wadau ikiwemo upungufu wa madawati, matundu ya vyoo  vyumba vya madarasa,uzio pamoja na kutokuwa na nyumba za walimu.

Kwa upande wao wahitimu wameiomba Serikali na wadau kuendelea kuchukua hatua za kukomesha ukatili dhidi ya watoto, wakieleza kuwa watoto wanahitaji mazingira salama ili waweze kusoma kutimiza ndoto zao na kufikia malengo yao ya maisha.

Wamesema mtoto anapopewa ulinzi, malezi bora na fursa ya elimu, anapata nafasi kubwa ya kujenga maisha yenye tija na kuwa raia mwema wa Taifa.

Naye Diwani wa Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga Jacline Isalo, amewataka wahitimu kuwatii wazazi na walezi wao, kuheshimu jamii na kuwa mfano mzuri katika maeneo wanayoelekea kuishi na kusoma.

Kwa ujumla, viongozi katika mahafali hayo wamewasisitiza wahitimu kuwa elimu, hofu ya Mungu, nidhamu, heshima kwa wazazi na kuchagua marafiki sahihi ni msingi muhimu wa kujenga maisha yenye mafanikio na kuwa viongozi bora wa kesho.


Mgeni rasmi katika mahafali ya 21 ya Shule ya Msingi Mapinduzi "B" diwani WA kata ya Chemchem wilayani Tabora Salum Bandora akizungumza


Diwani wa kata ya Ngokolo Jacklini Isalo akizungumza kwenye mahafali a darasala Saba mapinduzi "B"

Mgeni rasmi katika mahafali ya 21 ya Shule ya Msingi Mapinduzi "B" diwani WA kata ya Chemchem wilayani Tabora Salum Bandora akikabidhi vyeti kwa mmoja wa wahitimu 
Mgeni rasmi katika mahafali ya 21 ya Shule ya Msingi Mapinduzi "B" diwani WA kata ya Chemchem wilayani Tabora Salum Bandora akikabidhiwa zawadi kutoka shule ya Mapinduzi "B"

Mdau wa elimu  Christian Msipi akizungumza kwenye mahafali hiyo ya Mapinduzi "B"
Mwenyekiti wa CCM kata ya Ngokolo akizungumza George Mwandu akizungumza
Wahitimu wa darasa la Saba katika shule hiyo wakimsikiliza mgeni rasm
Wanafunzi wakiendelea na burudani









Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464