Aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Mkuu Angelo Accattino, amesifu amani, utulivu na mshikamano uliopo nchini, akieleza kuwa taifa hilo limejengwa katika misingi thabiti inayotokana na ushirikiano mzuri baina ya serikali na taasisi za dini.
Askofu Mkuu Accattino aliyasema hayo katika Viwanja vya Msimbazi, Dar es Salaam, wakati wa sherehe za kuwekwa wakfu kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Vincent Mpwaji. Alisema kuwa licha ya Tanzania kuwa na makabila na dini mbalimbali, wananchi wake wameendelea kudumisha mshikamano mkubwa na kuishi kwa upendo kwa ajili ya ustawi wa jamii.
Katika utume wake uliodumu kwa takribani miaka mitatu na nusu tangu alipoteuliwa Januari 2, 2023, kiongozi huyo alisema amejifunza na kushuhudia ukarimu wa pekee kutoka kwa Watanzania. Aliongeza kuwa Vatican inatambua na kuthamini ushirikiano uliopo kati ya serikali na kanisa, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kulinda na kudumisha amani hiyo kama tunu kuu waliyopewa na Mungu.
Akitolea mfano uwepo wa viongozi wa serikali katika maadhimisho hayo, alisema kuwa ushiriki huo ni kielelezo tosha cha uhusiano thabiti uliopo kati ya pande zote mbili. Katika kuaga kwake, Askofu Mkuu Accattino alibainisha kuwa hatasahau upendo mkubwa alioupata kutoka kwa Watanzania, akisema kuwa Dar es Salaam imekuwa nyumbani kwake na kwamba atakosa mambo mbalimbali ikiwemo samaki wabichi wa baharini na uchangamfu wa wananchi.
"Hakika nitaukosa upendo wa Watanzania kwani haya ni maadhimisho yangu ya mwisho ninayoshiriki leo kama Mwakilishi wa Kitume wa Baba Mtakatifu kwani leo usiku naondoka, naenda kufanya utume Colombia ambapo nimeteuliwa na Kiti Kitakatifu kuwa Balozi wa Vatican nchini humo," alisema.
Agosti 15 mwaka huu, Baba Mtakatifu Leo XIV alimteua Askofu Mkuu Accattino kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Colombia, hatua inayohitimisha kipindi chake cha utume hapa nchini Tanzania.
