` ALGERIA YAAHIDI USHIRIKIANO SEKTA YA VIWANDA VYA DAWA

WANDAMAN HOTEL

ALGERIA YAAHIDI USHIRIKIANO SEKTA YA VIWANDA VYA DAWA


Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria imesema itahakikisha inaiwezesha Tannzania kuwa na utaalamu wa kisasa wa utengenezaji wa dawa na vifaa vya tiba.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda vya Dawa wa Algeria, Dkt. Wassim Kouidri, katika ofisi za wizara hiyo jijini Algiers wakati wa mazungumzo ya waziri huyo na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi.

Mazungumzo hayo yalihusu namna ya kuimarisha ushirikiano zaidi katika sekta ya viwanda vya dawa ambayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeazimia kuiendeleza ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani Tanzania na la ukanda wa Afrika.

Katika mazungumzo hayo Balozi Matinyi alimweleza Waziri Kouidri kwamba Serikali ya Tanzania hivi sasa imeweka vivutio maalum kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya viwanda vya dawa nchini na tayari kuna viwanda vitano vinavyoendelea kujengwa na vingine zaidi vinatarajiwa.
Balozi Matinyi alielezea nia ya Serikali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda vya dawa na vifaa vya tiba katika ukanda wa nchi za mashariki, kati na kusini mwa Afrika wenye watu takriban milioni 350.

Algeria inaheshimika katika sekta ya viwanda vya dawa na vifaa vya tiba kwa kuwa na jumla ya viwanda 230, ikiwa ni theluthi moja ya viwanda vyote 690 barani Afrika.

“Ni kweli, Tanzania ipo kwenye eneo zuri la kimkakati la ukanda mkubwa wa Afrika na Algeria iko tayari kushirikiana nayo kitaalamu ili kuhakikisha inafikia malengo yake,” alisema Waziri Kouidri.

Aidha, Balozi Matinyi pia aliikaribisha nchini Mamlaka ya Taifa ya Bidhaa za Dawa (ANPP) ya Algeria ambayo inatazamiwa kuja nchini mwezi Oktoba mwaka huu kwa mwaliko wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) kujadili namna bora ya kushirikiana katika masuala ya kitaalam.

Tanzania inaheshimika barani Afrika kwa kuwa nchi ya kwanza kufikia kiwango cha daraja la tatu la ukaguzi wa dawa (ML3) mwaka 2018 chini ya tathmini ya viwango (GBT) ya Shirika la Afya la Dunia (WHO), ambayo hupima ubora wa ukaguzi wa dawa katika mifumo ya nchi.

Tangu mwaka 2020 nchi zingine tisa za Afrika zimefikia kiwango hicho cha ML3 huku kukiwa hakuna iliyofikia daraja la ML4 ambalo ni la juu zaidi. Nchi hizo mbali ya Tanzania ni Afrika Kusini, Ethiopia, Ghana, Misri, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Senegal na Zimbabwe.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464