` TRA YAZINDUA KLABU YA KODI SHULE YA WASICHANA SHINYANGA

WANDAMAN HOTEL

TRA YAZINDUA KLABU YA KODI SHULE YA WASICHANA SHINYANGA

 

Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Maro, akiwa pamoja na Mkuu wa Shule ya Wasichana Shinyanga, Mwalimu Nurah Kamuntu, wakati wa uzinduzi rasmi wa Klabu ya Kodi katika shule hiyo, Agosti 17, 2026. Picha na Elizabeth Cosmas
Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Maro, akiwa pamoja na Mkuu wa Shule ya Wasichana Shinyanga, Nurah Kamuntu, wakati wa uzinduzi rasmi wa Klabu ya Kodi katika shule hiyo, Agosti 17, 2026.

Na Elizabeth Cosmas, SHINYANGA

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imezindua rasmi Klabu ya Kodi katika Shule ya Wasichana Shinyanga 'Shinyanga Girls Secondary School', ikiwa na lengo la kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa kodi, sheria na sera za kodi, pamoja na kuwahamasisha kuwa mabalozi wa elimu ya kodi katika jamii.

Uzinduzi huo umefanyika leo, Agosti 17, 2026, katika Shule ya Wasichana Shinyanga na umefanywa na Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Maro, ambaye amesema kuanzishwa kwa klabu hiyo ni sehemu ya juhudi za TRA kuwafikia vijana wakiwa shuleni na kuwajengea uelewa wa masuala ya kodi tangu wakiwa katika hatua za awali za elimu.

Maro amesema kupitia klabu hiyo, wanafunzi watapata fursa ya kujifunza kuhusu kodi na umuhimu wake katika maendeleo ya nchi, huku wakitarajiwa kutumia elimu watakayoipata kuwaelimisha wanafunzi wenzao na jamii inayowazunguka.
“Napenda kuupongeza uongozi wa Shule ya Wasichana Shinyanga kwa kutambua umuhimu wa klabu hii na kutupokea ili kuifungua rasmi. Imani yetu ni kwamba baada ya wanachama kupata mafunzo stahiki kuhusu mchakato mzima wa ulipaji kodi, watakuwa mabalozi wazuri baada ya kuhitimu masomo yao,” amesema Maro.

Amesema elimu ya kodi inayotolewa kupitia klabu hizo haipaswi kubaki kwa wanachama pekee, bali inapaswa kusambaa kwa wanafunzi wengine na jamii kwa ujumla ili kuongeza uelewa kuhusu wajibu wa kulipa kodi na mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kiutawala nchini.

Aidha, Maro amemtunuku cheti cha pongezi Mkuu wa Shule ya Wasichana Shinyanga, Nurah Kamuntu, kwa kutambuliwa kuwa mhamasishaji bora, sambamba na kutoa zawadi za vyombo vya muziki kwa wanachama wa klabu hiyo kwa ajili ya kuwasaidia katika shughuli zao mbalimbali, ikiwemo midahalo.
Maro amewataka wanachama wa klabu hiyo kutumia elimu watakayoipata kama fursa ya kuelimisha jamii na kuhakikisha maarifa hayo hayabaki kwa matumizi yao binafsi.

Kwa upande wake, Mlezi wa Klabu ya Kodi, Omary Kiungi, amesema klabu hiyo ilianzishwa rasmi Januari 1, 2026, huku uzinduzi wake rasmi ukifanyika Agosti 17, 2026.

Kiungi amesema kwa sasa klabu hiyo ina zaidi ya wanachama 200, wakiwemo wanafunzi pamoja na baadhi ya walimu wa shule hiyo.

“Klabu hii ilianzishwa rasmi Januari 1, 2026, ikiwa na lengo la kujifunza njia za ulipaji kodi na elimu yake kwa ujumla. Leo klabu imefunguliwa rasmi na mpaka sasa tuna jumla ya wanachama zaidi ya 200, wakiwemo wanafunzi na baadhi ya walimu wa shule hii,” amesema Kiungi.

Amesema uwepo wa Klabu ya Kodi shuleni unawapa wanafunzi fursa ya kujifunza mapema kuhusu wajibu wa kulipa kodi na namna kodi inavyohusiana na maendeleo ya nchi, jambo litakalowasaidia kuwa raia wenye uelewa wanapohitimu na kuingia katika shughuli za kiuchumi.
Kiungi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mkazo katika utoaji wa elimu ya kodi na kuingiza masuala hayo katika mitaala ya masomo ya biashara.

Amesema hatua hiyo inawapa wanafunzi nafasi ya kupata elimu ya kodi wakiwa shuleni na kuwaandaa mapema kuelewa wajibu wao wa kulipa kodi watakapokuja kufanya kazi au kuanzisha biashara.

Baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, akiwemo Agness William na Antonia Yusuph, wamesema kuanzishwa kwa Klabu ya Kodi kutawasaidia kuelewa kwa undani mchakato wa ulipaji kodi na umuhimu wake katika maendeleo ya nchi.

Wamesema elimu watakayoipata kupitia klabu hiyo wataitumia kuwaelimisha wanafunzi wenzao ambao bado hawajajiunga na klabu, pamoja na jamii inayowazunguka.

Aidha, wamesema klabu hiyo itawajengea uzalendo na kuwasaidia kuelewa wajibu wao kwa Taifa, hasa watakapohitimu masomo na kuanza kushiriki katika shughuli za kiuchumi, ikiwemo ajira na biashara.
Kuanzishwa kwa Klabu ya Kodi katika Shule ya Wasichana Shinyanga, TRA Mkoa wa Shinyanga inalenga kuwafikia vijana wakiwa katika hatua za awali za elimu, kuwajengea uelewa kuhusu kodi na kuendeleza utamaduni wa kutambua na kutekeleza wajibu wa kulipa kodi.

Wanafunzi hao pia wanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuifikisha elimu ya kodi kwa wanafunzi wenzao, familia na jamii kwa ujumla, hivyo kuchangia kujenga kizazi chenye uelewa wa wajibu wa kodi na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa za TRA kuhusu Klabu za Kodi, klabu hizo hutumika kama jukwaa la kukuza uelewa wa kodi miongoni mwa wanafunzi, huku shughuli zake zikihusisha semina, mijadala na mashindano mbalimbali yanayolenga kupima na kuimarisha uelewa wa wanafunzi kuhusu kodi, sheria na sera za kodi.

Kupitia shughuli hizo, wanafunzi hupewa nafasi ya kujadili masuala ya kodi, kubadilishana uelewa na kujenga uwezo wa kueleza umuhimu wa kodi katika maendeleo ya nchi. Hatua hiyo pia huwajenga kuwa mabalozi wa elimu ya kodi wanapokuwa shuleni na hata baada ya kuhitimu.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464