` TCB, TACOEJ WAWAJENGEA UWEZO WA WAANDISHI KUANDIKA HABARI ZA PAMBA KWA USAHIHI

WANDAMAN HOTEL

TCB, TACOEJ WAWAJENGEA UWEZO WA WAANDISHI KUANDIKA HABARI ZA PAMBA KWA USAHIHI

Afisa Kilimo wa Bodi ya Pamba Tanzania Kanda ya Magharibi, Penina Range, akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu uandishi na uripoti wa habari za zao la pamba, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bodi ya Pamba, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026. 
  Washiriki wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wakitembelea Maabara ya Usanifu wa Madaraja ya Pamba iliyopo katika Ofisi za Bodi ya Pamba Tanzania, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1  blog
Katibu wa Waandishi wa Habari za Pamba na Mazingira (TACOEJ), Sitta Tuma, akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu uandishi na uripoti wa habari za zao la pamba yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bodi ya Pamba, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026.
Afisa Kilimo na Uhamasishaji wa Zao la Pamba, Edward Nyawile, akiwasilisha mada wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu uandishi na uripoti wa habari za zao la pamba, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bodi ya Pamba, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026.
Afisa Kilimo anayeshughulikia upande wa Maabara kutoka Bodi ya Pamba Tanzania, Doto Ntumba, akitoa mada kuhusu usafi na ubora wa pamba wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bodi ya Pamba, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026.
Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu uandishi na uripoti wa habari za zao la pamba, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bodi ya Pamba, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026.

Na Kadama Malunde, Malunde 1 blog

Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), kwa kushirikiana na Waandishi wa Habari za Pamba na Mazingira (TACOEJ), imeendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kutoka mikoa mitano, kwa lengo la kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu namna sahihi ya kuandika na kuripoti habari za zao la pamba.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bodi ya Pamba, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026 yamelenga kuwawezesha waandishi wa habari kupata uelewa mpana kuhusu sekta ya pamba, changamoto zinazowakabili wakulima, hatua zinazochukuliwa na Serikali pamoja na namna bora ya kutumia habari kama chombo cha kutoa elimu na kuhamasisha ongezeko la tija katika uzalishaji wa zao hilo.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Kanda ya Magharibi, Afisa Kilimo wa Bodi ya Pamba, Penina Range, amewataka waandishi wa habari kuzingatia weledi, usahihi na taaluma wakati wa kuandika na kuripoti habari zinazohusu pamba.

Penina amesema waandishi wanapaswa kutumia taarifa sahihi kutoka vyanzo vinavyoaminika, hususan Bodi ya Pamba, ili kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi inayoweza kuwasaidia kuongeza tija katika uzalishaji.

“Kupitia mafunzo haya mkawe mabalozi wa kuelimisha wakulima ili kuongeza tija ya uzalishaji wa pamba. Wakulima wengi wanahitaji elimu sahihi kutoka kwa waandishi wa habari. Andikeni kwa usahihi, weledi na kuzingatia taaluma zenu,” amesema Penina.
Afisa Kilimo wa Bodi ya Pamba Tanzania Kanda ya Magharibi, Penina Range.

Amesema waandishi wa habari wanapaswa kujenga utamaduni wa kuwasiliana na Bodi ya Pamba pale wanapokuwa na mashaka kuhusu taarifa wanayotaka kuichapisha au kuitangaza, ili kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu.

“Tuwe mabalozi. Kama unahisi unachokitoa huna usahihi nacho, tuwasiliane na Bodi ya Pamba kwa sababu viongozi wapo na watatoa ushirikiano muda wote. Tunataka kuwa kiunganishi baina yetu na wadau wa pamba; hatuna uwezo wa kuwafikia wadau wote bila nyie,” amesema.

WAANDISHI WANA MCHANGO MKUBWA SEKTA YA PAMBA

Awali, akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Afisa Kilimo na Uhamasishaji wa Zao la Pamba, Edward Nyawile, amesema waandishi wa habari wana mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ndogo ya pamba, kwa kuwa wana uwezo wa kufikisha taarifa na elimu kwa wakulima na wadau wengi kwa wakati mmoja.
Nyawile amesema zao la pamba linasimamiwa chini ya Sheria ya Pamba Na. 2 ya mwaka 2001, huku Serikali kupitia Bodi ya Pamba ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima.

Amesema Serikali kupitia Bodi ya Pamba imenunua matrekta 680 kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kurahisisha shughuli za kilimo na kupunguza utegemezi wa jembe la mkono.

Aidha, amesema Bodi imeanza kusajili wakulima katika mfumo wa kidijitali kwa lengo la kuwa na kanzidata itakayosaidia katika upangaji na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya zao la pamba.

Nyawile pia amesema maandalizi yamefanyika kwa ajili ya kuanzishwa kwa ekari 1,000 za kongani za viwanda katika eneo la Misungwi, hatua inayolenga kuongeza thamani ya zao la pamba na kuchochea shughuli za uchakataji na viwanda.

USAFI NA UBORA WA PAMBA

Akitoa mada kuhusu usafi na ubora wa pamba, Afisa Kilimo anayeshughulikia upande wa Maabara kutoka Bodi ya Pamba, Doto Ntumba, amesema Tanzania ina maabara moja ya usanifu wa pamba iliyopo Shinyanga, ambayo pia inahudumia nchi za Kenya na Uganda.
Amesema bado kuna changamoto katika kuhakikisha pamba inayozalishwa na wakulima inakuwa safi na yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko, kutokana na baadhi ya wakulima kuchanganya pamba na uchafu wakati wa uvunaji, uhifadhi na usafirishaji.

Doto amesema maabara hiyo ina vitengo vya usanifu wa pamba kwa kutumia mikono pamoja na mashine, ambapo wataalamu hupokea sampuli za pamba na kufanya uchunguzi kwa ajili ya kubaini na kutoa madaraja ya ubora wa pamba.

“Hapa tuna maabara za aina mbili, maabara ya usanifu wa mikono na maabara ya usanifu wa mashine. Wataalamu wetu wanapokea sampuli na kutoa madaraja ya pamba. Wakulima wakielimika, nasi tutaweza kuwa na pamba safi na tutauza kwenye soko, na pamba yetu itanunuliwa kwa wingi sana. Waandishi wa habari mna mchango mkubwa kuhakikisha tunapata pamba safi,” amesema Doto.

Amesema waandishi wa habari wana nafasi muhimu katika kutoa elimu kuhusu namna bora ya kuvuna, kuhifadhi na kusafirisha pamba ili kupunguza uchafuzi na kuongeza thamani ya zao hilo katika soko.

TACOEJ: PAMBA INALIMWA MIKOA 17

Kwa upande wake, Katibu wa TACOEJ, Sitta Tuma, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari kwa kuwa yanawaongezea maarifa na uwezo wa kuripoti na kuandika habari zinazohusu zao la pamba kwa usahihi na weledi.

Amesema zao la pamba linalimwa katika mikoa 17 nchini, hivyo ni muhimu waandishi wa habari wanaoripoti kutoka maeneo hayo kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sekta hiyo ili waweze kutoa taarifa zenye manufaa kwa wakulima na wadau wengine.

Amesema TACOEJ itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kutumia taaluma yao kuelimisha jamii na kuchochea uzalishaji wenye tija katika zao la pamba.

WAKULIMA WAPEWE ELIMU ZAIDI

Kwa upande wake, Moshi Ndugulile, Mwandishi wa Habari na Mtangazaji kutoka Faraja FM, amesema mafunzo hayo yamewapa waandishi uelewa muhimu ambao utawasaidia kuripoti masuala ya pamba kwa kina na kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wakulima.

Amesema wakulima wa pamba wanahitaji kupewa elimu ya kutosha kuhusu kanuni bora za kilimo, uvunaji, uhifadhi na utunzaji wa zao hilo ili kuongeza uzalishaji na ubora.

Ndugulile amesema waandishi wa habari wanapaswa kutumia nafasi yao kuibua changamoto zinazowakabili wakulima, kutoa elimu sahihi na kuonyesha fursa zilizopo katika sekta ya pamba ili kusaidia kurejesha uzalishaji wa zao hilo katika viwango vya juu.

Amesema pamba imewahi kuitwa “Dhahabu Nyeupe” kutokana na umuhimu wake kiuchumi, hivyo juhudi za pamoja za Serikali, wakulima, wadau wa sekta na vyombo vya habari zinahitajika ili kuongeza tija, ubora na thamani ya zao hilo.

Mafunzo hayo yamewakutanisha waandishi wa habari kutoka mikoa inayozalisha pamba, ambapo wamepata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu uzalishaji, usafi na ubora wa pamba, sera na sheria zinazosimamia zao hilo pamoja na nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha na kuhamasisha wakulima.
Afisa Kilimo wa Bodi ya Pamba Tanzania Kanda ya Magharibi, Penina Range, akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu uandishi na uripoti wa habari za zao la pamba, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bodi ya Pamba, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026.


Katibu wa Waandishi wa Habari za Pamba na Mazingira (TACOEJ), Sitta Tuma, akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu uandishi na uripoti wa habari za zao la pamba yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bodi ya Pamba, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026.





Washiriki wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wakitembelea Maabara ya Usanifu wa Madaraja ya Pamba iliyopo katika Ofisi za Bodi ya Pamba Tanzania, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026.
Washiriki wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wakitembelea Maabara ya Usanifu wa Madaraja ya Pamba iliyopo katika Ofisi za Bodi ya Pamba Tanzania, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026.
Washiriki wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wakitembelea Maabara ya Usanifu wa Madaraja ya Pamba iliyopo katika Ofisi za Bodi ya Pamba Tanzania, Mjini Shinyanga, Agosti 17, 2026.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464