` BENKI KUU YA TANZANIA YATANGAZA UCHUMI KUENDELEA KUIMARIKA

WANDAMAN HOTEL

BENKI KUU YA TANZANIA YATANGAZA UCHUMI KUENDELEA KUIMARIKA


Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuwa kiwango cha fedha zinazozunguka kwenye uchumi kimefika Shilingi trilioni 10, huku ukwasi wa fedha katika mabenki ukifikia Shilingi trilioni 6.2 kutoka Shilingi trilioni 1.6 ilivyokuwa miaka michache iliyopita, hali inayodhihirisha kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini.
Akizungumza kwenye kipindi maalumu cha kuadhimisha miaka 60 ya BoT kupitia kituo cha TBC1, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alisema kuwa ongezeko hilo linachochewa na kuimarika kwa biashara, uzalishaji, na upatikanaji wa fedha za kutosha zinazowezesha wananchi kubadilishana bidhaa na huduma kwa ufanisi mkubwa.

Alisisitiza kuwa benki itaendelea kusimamia sera za fedha ili kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki katika kiwango salama cha asilimia tatu hadi tano, huku akibainisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye mfumuko wa chini wa bei katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa, ikiwemo kuongeza kiwango cha riba ya Benki Kuu hadi asilimia 6.2.

Katika upande wa akiba ya taifa na utulivu wa sarafu, Gavana Tutuba alifafanua kuwa tangu kuanzishwa kwa mpango wa kununua dhahabu Oktoba 2024, BoT imehifadhi tani 29 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi trilioni 11, hatua iliyosaidia kupunguza utoroshaji wa madini, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, na kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya misukosuko ya kiuchumi ya kimataifa.

Alieleza kuwa thamani ya Shilingi imekuwa himilivu sana ukilinganishwa na nchi za ukanda huu, ikionesha kupoteza thamani kwa asilimia ndogo tu ya takriban asilimia 0.1 katika miezi mitatu iliyopita na asilimia 3.3 kutoka Julai 2025 hadi Julai 2026.
Ili kuendelea kuimarisha soko la fedha za kigeni na kurahisisha upatikanaji wake kwa wafanyabiashara, BoT imeweka madaraja matatu ya maduka ya kubadilisha fedha kulingana na mitaji na maeneo ya biashara, ambapo hadi sasa leseni 202 zimetolewa.

Aidha, Gavana Tutuba alikumbusha kuwa Kifungu cha 26 cha Sheria ya BoT ya Mwaka 2006 kinasisitiza matumizi ya Shilingi ya Tanzania kama fedha halali kwa miamala yote ya ndani, jambo ambalo limefanikiwa kuacha fedha za kigeni kwa ajili ya mahitaji maalumu kama vile uagizaji wa dawa na mitambo, huku akibainisha kuwa mchakato wa kufikia sarafu moja ya Afrika Mashariki unaendelea vyema kwa kuzingatia vigezo vya pamoja vya kiuchumi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464