` VIJANA NA WAJIBU WA KULINDA AMANI KAMA MTAJI WA MAENDELEO YA TAIFA

WANDAMAN HOTEL

VIJANA NA WAJIBU WA KULINDA AMANI KAMA MTAJI WA MAENDELEO YA TAIFA

Vijana wana jukumu kubwa la kulinda amani ya nchi, kwani wao ndio nguvu kazi ya Taifa na viongozi wa kesho. 

Kwa wingi wao, ubunifu wao na ushawishi wao katika jamii, kundi hili lina nafasi ya kipekee ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa lenye umoja, utulivu na maendeleo. 

Hivyo, hawapaswi kabisa kukubali kutumiwa kwa namna yoyote ile kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ambayo imeendelea kuwa tunu ya Taifa kwa miongo mingi.

Amani ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya sekta zote muhimu nchini. 

Bila uwepo wa amani hakuna biashara zinazoweza kustawi, uwekezaji kutoka ndani na nje hupungua kwa kiasi kikubwa, na shughuli zote za uzalishaji mali husimama.

 Aidha, hali ya machafuko husababisha watoto kukosa fursa ya kupata elimu na huduma za afya huathirika kwa kiwango cha juu, jambo linalothibitisha kuwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii hayawezi kupatikana bila mazingira ya utulivu na usalama.

Historia ya baadhi ya mataifa yaliyokumbwa na migogoro inatoa funzo muhimu sana kwetu.

 Kukosekana kwa amani kumesababisha wananchi wengi kupoteza maisha, mali na makazi, huku wengine wakilazimika kuyahama maeneo yao ili kutafuta usalama ukimbizini. 

Katika mazingira hayo, shule zimefungwa, huduma za afya zimedorora, uchumi umesimama na ndoto za mamilioni ya vijana zimekatishwa kabisa, mafunzo ambayo yanapaswa kuwafanya vijana wa Tanzania kuthamini na kuilinda amani waliyonayo sasa.

Katika dunia ya sasa ya kidijitali, mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

 Ingawa imeleta fursa nyingi za elimu, biashara na mawasiliano, wakati mwingine imekuwa ikitumiwa kusambaza taarifa zisizo sahihi na ujumbe unaoweza kuleta taharuki au migawanyiko.

 Hivyo basi, vijana wanapaswa kutumia busara kubwa katika majukwaa hayo kwa kuhakiki taarifa kabla ya kuzisambaza na kuhakikisha wanatumia sauti zao kuhamasisha umoja, mshikamano na maendeleo ya nchi yao.

Mchango wa vijana katika kujenga Taifa unapaswa kuonekana zaidi kupitia elimu, ujasiriamali, teknolojia, kilimo, sanaa na ubunifu. 

Nguvu zao zote zinapaswa kuelekezwa katika kuzalisha fursa mpya na kutatua changamoto za maendeleo badala ya kushiriki au kushawishiwa kuingia kwenye vitendo vinavyoweza kuhatarisha mustakabali wao na wa Taifa kwa ujumla.

Ni dhahiri kuwa kulinda amani si jukumu la vyombo vya dola pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania.

 Vijana wanapaswa kuwa mabalozi wa kwanza wa amani kwa kuhamasisha mazungumzo yenye staha, kuheshimu sheria za nchi na kukataa kabisa kushawishiwa kufanya vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa jamii yetu.

Tanzania imebarikiwa kuwa miongoni mwa mataifa machache yanayojivunia amani, umoja na mshikamano wa dhati.

 Ni wajibu wa kila kijana kuhakikisha kuwa urithi huo wa thamani unaendelea kudumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo, kwani amani yetu ndio mtaji wetu mkubwa unaopaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464