` JAB YAZINDUA RASMI MWONGOZO WA KISHERIA WA UTOAJI WA ITHIBATI YA MAISHA KWA WAANDISHI WA HABARI WAKONGWE

WANDAMAN HOTEL

JAB YAZINDUA RASMI MWONGOZO WA KISHERIA WA UTOAJI WA ITHIBATI YA MAISHA KWA WAANDISHI WA HABARI WAKONGWE


Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imezindua rasmi Mwongozo wa Kisheria wa Utoaji wa Ithibati ya Maisha kwa Waandishi wa Habari Wakongwe, hatua inayolenga kutambua na kuthamini mchango wa waandishi wa habari waliolitumikia Taifa kwa muda mrefu na kwa utumishi uliotukuka katika maendeleo ya sekta ya habari nchini.

Uzinduzi huo umefanyika leo, Julai 11, 2026, wakati wa maadhimisho ya JAB Day yaliyofanyika katika Banda la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Kupitia hotuba yake iliyosomwa na Dkt. Egbert Mkoko, Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Bw. Tido Mhando, alisema mwongozo huo umeandaliwa kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa Bodi chini ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 pamoja na Kanuni zake, ili kuweka utaratibu wa utoaji wa Ithibati ya Maisha kwa waandishi wa habari wakongwe waliotoa mchango wa kipekee katika maendeleo ya taaluma hiyo.

Alisema mwongozo huo unawahusu waandishi wa habari ambao wakati Sheria ya Huduma za Habari ilipoanza kutumika mwaka 2016 walikuwa na umri wa miaka 50 au zaidi na walikuwa tayari wametoa mchango mkubwa katika sekta ya habari, lakini hawakupata fursa ya kujiendeleza hadi kufikia sifa za kitaaluma zinazohitajika kwa mujibu wa sheria.

"Mwongozo huu unalenga kuhifadhi historia ya tasnia ya habari, kuthamini mchango wa waandishi wa habari wakongwe na kuhakikisha uzoefu wao unaendelea kuwa sehemu ya urithi wa taaluma ya uandishi wa habari nchini," ilieleza sehemu ya hotuba ya Mwenyekiti.

Bw. Mhando alisisitiza kuwa mwongozo huo hauondoi wala haupunguzi masharti ya msingi yaliyowekwa na Sheria ya Huduma za Habari kuhusu sifa za kupata ithibati kwa waandishi wa habari, bali unaweka utaratibu wa kutekeleza mamlaka ambayo sheria imeipa Bodi kuhusu utoaji wa Ithibati ya Maisha kwa watu wenye utumishi uliotukuka na waliotoa mchango wa kipekee katika maendeleo ya sekta ya habari.

Aidha, aliipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kuiwezesha Bodi kutekeleza majukumu yake.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464