Na Marco Maduhu, SHINYANGA
IDARA ya huduma ya vijana kutoka Kanisa la
Waadventista Wasabato Mtaa wa Lubaga uliopo Manispaa ya Shinyanga, wamefanya
utalii wa ikolojia katika Hifadhi ya Msitu wa Lubaga mjini hapa, kwa lengo la
kujifunza masuala mbalimbali ya mazingira na asili.
TAZAMA VIDEO HAPA👇👇
Utalii huo umefanyika leo Julai 5, 2026 ambapo mbali na kujifunza mambo hayo ya asili, vijana hao walipata fursa ya kuburudika kwa michezo ya kubembea pamoja na kujionea wanyama aina ya ngedere wanaopatikana katika hifadhi hiyo.
Akizungumza mmoja wa vijana walioshiriki utalii
huo, Benjamini Martine, amesema ziara hiyo imekuwa na tija kubwa kwao ambapo
wameweza kujifunza mambo mengi kwa vitendo.
"Tumejifunza vitu vingi vya asili
ikiwamo kuona matunda pori, miti ya dawa, na namna nyuki wanavyoishi,
wanavyotengeneza asali pamoja na mbinu bora za ufugaji wa nyuki hao,"
amesema Martine.
Naye Kiongozi wa Idara ya huduma ya vijana wa
kanisa hilo, Jackson Sadick, amesema lengo la kufanya utalii huo wa ndani ni
kuwajenga watoto na vijana kuelewa rasilimali za asili zilizopo ndani ya nchi.
Ameongeza
kuwa katika ziara hiyo, wamejionea aina ya miti zaidi ya 300 , ikiwamo ya sumu,
matunda, na ile inayofaa kwa tiba asilia.
Kwa
upande wake msimamizi wa hifadhi ya msitu wa Lubaga, Wille Shuli , amesema
wameamua kuanzisha na kuhamasisha utalii huo wa ikolojia, ili kutoa fursa kwa
wananchi na familia zao kufanya utalii wa ndani karibu na maeneo yao, huku
wakipata fursa ya kufurahi na kujifunza mambo ya kiasili.
TAZAMA PICHA👇👇