` SERIKALI YASISITIZA UTAYARI WAKE MCHAKATO WA KATIBA MPYA

WANDAMAN HOTEL

SERIKALI YASISITIZA UTAYARI WAKE MCHAKATO WA KATIBA MPYA


Serikali imesisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kuwa watulivu, kulinda amani, na kuunga mkono juhudi za ujenzi wa taifa.

Aidha imesema kwamba yenyewe iko tayari kuendeleza mjadala na mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya kwa maslahi mapana ya nchi. 

Akizungumza leo Julai 24, 2026, katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) uliofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewahimiza wananchi na wadau mbalimbali kujenga umoja na mshikamano ili kuondoa migawanyiko na kuepuka uhasama usio na tija kwa taifa.

Makamu wa Rais aliwahimiza Watanzania kuendelea kuonyesha dhamira na kuongeza juhudi katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, akieleza kuwa mapendekezo kutoka Tume ya Haki Jinai na Tume ya Jaji Chande yameweka misingi thabiti inayooana na nia ya dhati ya serikali kuendeleza ajenda hiyo muhimu kwa ustawi wa demokrasia na utawala bora nchini.

Katika mkutano huo, Dkt. Nchimbi alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa mashirika na watetezi wa haki za binadamu, ikiwemo ushiriki wao katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyowafikia mamilioni ya wananchi. 

Alisisitiza kuwa endapo zitatokea tofauti za mitazamo, njia sahihi ya kuzitatua ni mazungumzo ya amani na kuheshimiana, akitolea mfano utayari wa viongozi kukaa pamoja na wanaharakati kwa kuwa tofauti za kifikra hazipaswi kamwe kuwa chanzo cha uadui.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464