Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wateule kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, ushirikiano na bila upendeleo, wakitanguliza huduma kwa wananchi na maslahi ya Taifa Alisema hayo Ikulu, Tunguu, Zanzibar, mara baada ya kuwaapisha Naibu Makatibu Wakuu wawili na kushuhudia viongozi wengine wanne wakila Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma.
Katika maagizo yake, Rais Dkt. Samia ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kuimarisha usimamizi wa masuala ya Muungano na kutatua changamoto zinazojitokeza, huku akiwataka viongozi kushirikiana kusimamia programu za uhifadhi wa mazingira na kuitaka Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuboresha mazingira ya utumishi kwa ufanisi.
Aidha, ameelekeza kuongezwa kasi katika sekta ya uchukuzi kupitia ujenzi na usimamizi wa miradi ya reli, barabara, bandari, meli na utathmini wa biashara ya anga ya ATCL, sambamba na kuiagiza Wizara ya Katiba na Sheria kuimarisha upatikanaji wa haki kupitia kampeni za msaada wa kisheria.
Katika kuimarisha taasisi za umma na uchumi wa taifa, Rais Dkt. Samia ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuboresha ukuzaji biashara na usimamizi wa maonesho, kuliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kulinda rasilimali za utalii na hifadhi za wanyamapori, na kulitaka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuimarisha ubora wa maudhui na weledi kama sauti ya Taifa.
Viongozi walioapishwa kushika nyadhifa hizo ni Dkt. Latifa Mohammed Khamis kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, na Bi. Prisca Burton Lwangili kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakati walioapa Kiapo cha Uadilifu ni Bw. Ephraim Balozi Mafuru (TANTRADE), Bw. Salum Nassor Mnuna (EWURA), Bw. Massana Gibril Mwishawa (TANAPA), na Bi. Asha Dachi Mbaruk (TBC).
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
