Jeshi la Polisi Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza limewataka vijana nchini kulinda amani na utulivu kwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya dola pamoja na serikali za mitaa ili kuwabaini na kuwafichua wahalifu wanaojificha ndani ya jamii, likisisitiza kuwa vijana ni nguzo kuu inayopaswa kusimama kidete kama mabalozi wa amani.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Virginia Sodoka, alitoa wito huo wakati wa fainali za mashindano ya Kombe la Polisi Jamii yaliyofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mirongo, ambapo timu ya Mashi FC iliibuka mabingwa wapya baada ya kuifunga Mirongo FC mabao 2-0.
Mkuu huyo wa polisi alionya kuwa pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kujenga taifa, vijana wanaweza pia kutumiwa vibaya na watu wenye nia ovu iwapo hawatakuwa makini na kupata maelekezo sahihi ya uzalendo.
Akisisitiza umuhimu wa usalama kuanzia ngazi ya chini, Sodoka alieleza kuwa ulinzi huanzia katika ngazi ya mtaa na kwamba ushirikiano thabiti kati ya wananchi, viongozi wa mitaa na Jeshi la Polisi ndio ngao ya kudumisha amani ya nchi, huku akibainisha kuwa mashindano hayo yamekuwa jukwaa bora la kuimarisha uhusiano mwema na wananchi, kukuza vipaji vya vijana na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maendeleo na ujasiriamali.
Mtazamo huo uliungwa mkono na Polisi Kata ya Mirongo, Mkaguzi wa Polisi Fatuma Mpinga, aliyeeleza kuwa michezo hiyo imekuwa nyenzo madhubuti ya kuwaunganisha vijana, kuwajengea nidhamu na kuimarisha ushirikiano unaosaidia kuifanya kata hiyo kuwa salama na yenye utulivu.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mirongo, Nurdin Anas Baji, alitoa pongezi za dhati kwa Jeshi la Polisi kwa kuandaa mashindano hayo yenye tija kwa jamii, akiwataka vijana kutokubali kamwe kupotoshwa na watu wenye nia mbaya ya kuvuruga amani, bali waendelee kuwa mstari wa mbele na mfano wa kuigwa katika kudumisha mshikamano, umoja na amani ya kudumu ambayo ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya nchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
