` KISWAHILI CHAJIIMARISHA KAMA DARAJA LA USHIRIKIANO NA UTAMBULISHO WA UTAMADUNI

WANDAMAN HOTEL

KISWAHILI CHAJIIMARISHA KAMA DARAJA LA USHIRIKIANO NA UTAMBULISHO WA UTAMADUNI

 

Na Mwandishi Maalumu (KAM), Paris 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amesema lugha ya Kiswahili imeendelea kuwa daraja la ushirikiano na utambulisho wa utamaduni wa Mwafrika kwenye majukwaa ya kimataifa.

Katika hotuba aliyoitoa akimwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika Makao Makuu ya shirika la UNESCO jijini Paris nchini Ufaransa,Dkt Nchemba amesema hatua inaibua fursa mbalimbali za kiuchumi.

“Lugha ya Kiswahili imeendelea kuwa utambulisho na utamaduni wa Mwafrika tangu ilipoasisiwa na kwamba lugha hii inatumika rasmi na wananchi wa Afrika Mashariki na ni moja ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika” alisema Dkt. Nchemba.

Pamoja na kuelezea fursa mbalimbali zinazoambatana na lugha hiyo Katika hotuba yake ameipongeza UNESCO kwa uamuzi wake wa kukienzi na kukiendeleza Kiswahili kwa kuwa na siku maalumu ya kuadhimisha lugha hiyo kila mwaka ifikapo Julai 7.

Dkt. Mwigulu alisema Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yanayofanyika kuenzi lugha hiyo inayokadiriwa kuwa na wazungumzaji zaidi milioni 500 duniani kote sasa inatumika kwenye nyanja za elimu, biashara, uchumi, utalii na teknolojia hasa akili unde.

Katika hafla hiyo Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba alizindua machapisho maalumu ikiwemo kamusi ya Kifaransa kwa Kiswahili, Kitabu cha Maneno na Misemo ya kila siku (Kiswahili- Kiingereza – Kihausa) na kitabu cha Waasisi wa Fasihi ya Kiswahili.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Prof Khaled El- Enany alieleza kuwa Kiswahili kimekuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa sekta za elimu, teknolojia ya mawasiliano, utafiti, biashara  na ubunifu kutokana na kuwa na wazungumzaji wengi ulimwenguni.

Prof. Enany ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza jitihada za kueneza na kukuza lugha hiyo duniani ambapo sasa utamaduni wake unaenea na kuchangia upatikanaji wa amani, umoja na ushirikiano miongoni mwa mataifa.

Akitoa taarifa kuhusu Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ambaye pia ni Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la UNESCO Balozi Said Yakub alisema jumla ya nchi 16 zimeshiriki kwenye kongamano la mwaka huu.

Balozi Yakub alisema Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili limefanyika Jijini Paris kuanzia tarehe 04 hadi 07 ambapo wadau wa lugha hiyo toka nchi mbalimbali walishiriki pamoja na kujadili mada za kitaaluma, maonesho ya kazi za sanaa na matembezi maalum ya kukienzi Kiswahili katika mitaa ya jiji la Paris. 

Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Ufaransa, Balozi wa Senegal nchini Ufaransa Mheshimiwa Pierre Faye alisema ni furaha kwa nchi za Afrika kushiriki hafla hii kwa umoja kwa kuwa lugha ya Kiswahili inatumika kote na kudhihirisha utamaduni wa Afrika.

“Tunaposheherekea siku hii tuendelee kuenzi mchango wa viongozi wa Afrika waliotumia Kiswahili kukuza umoja wa Afrika” alihitimisha salamu zake Balozi Faye.

Maadhimisho ya mwaka huu yaliongozwa na kauli mbiu isemayo “Kiswahili ni Tunu kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi Duniani”.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464