Na Prosper Makene 

Tanzania imezitaka Nchi Duniani kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo na usimamizi wa Akili Unde (AI) ili kuhakikisha mataifa yote yananufaika kwa usawa na fursa zinazotokana na teknolojia hiyo.

Wito huo umetolewa leo tarehe 6 Julai, 2026 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Mbelwa Kairuki (Mb), wakati akiwasilisha tamko la Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Majadiliano kuhusu Utawala wa Akili Unde (Global Dialogue on AI Governance) unaofanyika mjini Geneva nchini Uswisi.

Mkutano huo ulifunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuweka mfumo wa utawala wa Akili Unde unaojumuisha mataifa yote, unaolinda haki za binadamu, unaojenga imani na kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kwa maendeleo endelevu na manufaa ya watu wote.

Akizungumza katika mkutano huo wenye washiriki zaidi ya 190 kutoka nchi mbalimbali duniani, Mhe. Kairuki alisema Serikali inaiona Akili Unde kuwa nyenzo muhimu ya kimkakati katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 pamoja na kukuza uchumi wa kidijitali.

Aliongeza kuwa, Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya AI kupitia uundaji wa mifumo ya utawala wa teknolojia hiyo, kuimarisha usimamizi wa data, ulinzi wa faragha na usalama wa mtandao, pamoja na kuandaa miongozo ya kitaifa ya matumizi ya AI katika sekta za elimu na afya.

"Tunaamini Akili Unde inaweza kuleta mageuzi makubwa katika sekta za kilimo, afya, elimu, huduma za kifedha na utawala wa umma, hivyo ni muhimu kuhakikisha teknolojia hii inatumika kwa njia salama, jumuishi na yenye manufaa kwa wananchi Wote” alisema Mhe. Kairuki.

Aidha, Waziri huyo alieleza kuwa Serikali ya Tanzania imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali ikiwemo upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na maendeleo ya Miundombinu ya Umma ya Kidijitali (Digital Public Infrastructure – DPI), hatua ambazo zitawezesha matumizi ya AI kufikia wananchi na sekta mbalimbali kwa usawa.

Mhe. Angellah Kairuki pia alieleza kuwa Tanzania inaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za kikanda na kimataifa ikiwemo ITU, Umoja wa Afrika (AU), African Telecommunications Union (ATU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kwa lengo la kuhakikisha mifumo ya kidijitali inaendana, inarahisisha biashara na uhamaji, huku ikiheshimu faragha na mamlaka ya kila nchi.

Akihitimisha hitimisho lake, Waziri Kairuki alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza ushirikiano katika kujenga uwezo wa wataalamu, kuhamisha teknolojia, kuendeleza tafiti za pamoja, kuimarisha mifumo ya ubunifu na kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya kidijitali, ili kuhakikisha hakuna taifa linaloachwa nyuma katika mapinduzi ya Akili Unde.

Mkutano wa Global Dialogue on AI Governance umewakutanisha viongozi wa serikali, watunga sera, wataalamu wa teknolojia, mashirika ya kimataifa na sekta binafsi kujadili mustakabali wa utawala wa Akili Unde duniani na namna ya kuhakikisha teknolojia hiyo inachangia maendeleo jumuishi, salama na endelevu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464