` KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AIPONGEZA HALMASHAURI YA MKALAMA KWA USIMAMIZI MZURI WA MIRADI YA MAENDELEO

WANDAMAN HOTEL

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AIPONGEZA HALMASHAURI YA MKALAMA KWA USIMAMIZI MZURI WA MIRADI YA MAENDELEO

 



Mkalama, Julai 26, 2026 – Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang'onda, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo baada ya kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi pamoja na programu mbalimbali yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.18.

Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Mwang'onda amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Moses Machali, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Hajjat Asia J. Messos, kwa usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha huduma za afya, maji, elimu, miundombinu na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Aidha, amewataka wananchi wa Wilaya ya Mkalama kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ili kuharakisha maendeleo ya Taifa.

Mwang'onda pia amesisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira, kuhifadhi misitu, kuboresha afya za wananchi na kuunga mkono ajenda ya Serikali ya matumizi ya nishati salama na endelevu.

Katika mbio hizo, Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa kwa umbali wa kilomita 143, ukizindua Kituo cha Afya Iguguno, kuweka jiwe la msingi la Daraja la Mawe la Upinde Kinyangiri na mradi wa maji, pamoja na kutembelea mradi wa kikundi cha vijana Tujikwamue Ndurumo, mradi wa barabara ya wananchi wa Mnolo, ujenzi wa nyumba ya kulala wageni Ibaga na mradi wa utengenezaji wa madawati kwa shule za sekondari wilayani Mkalama.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464