
Brigedia Jenerali mstaafu Wilfred Kabunda amewataka Watanzania, hususan vijana, kuendelea kuipenda na kuilinda nchi kwa uzalendo mkubwa.
“Niwasihi Watanzania, hususan vijana wa taifa hili, wawe wazalendo kwa nchi yao kwa sababu hatuna Tanzania nyingine, ni hii tuliyonayo. Tutunze amani tuliyonayo kwa wivu mkubwa sana,” alisema.
Jenerali Kabunda, alisema hayo katika Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, Julai 25 katika uwanja wa mashujaa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma baada ya kukamilika kwa shughuli za kuwakumbuka mashujaa zilizoongozwa na rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliweka mkuki na ngao katika mnara wa mashujaa.
Jenerali kabunda ambaye alikuwa mwakilishi wa mashujaa waliopigana Vita ya Kagerahivyo kuweka shoka katika adhimisho hilo , akiwa miongoni mwa makomandoo waliopigana Vita ya Kagera, alisema mafanikio ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika vita hiyo yalitokana na maandalizi madhubuti ya mafunzo na mshikamano wa Watanzania wote.
Alisema Brigade 208 ilikuwa imepata mafunzo ya kutosha kabla ya kuingia vitani, hali iliyowapa uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Mbali na mafunzo, hamasa ya Watanzania ilikuwa kubwa. Kila Mtanzania aliunga mkono vita hiyo na kujitolea kwa namna mbalimbali. Hilo lilitupa nguvu na morali ya kupambana hadi ushindi ukapatikana,” alisema.
Kwa upande wake, Brigedia Jenerali mstaafu Mary Hiki alisimulia namna alivyoshiriki Vita ya Kagera akiwa mwanamke pekee katika kundi la mawasiliano.
Alisema Oktoba mwaka 1978 alikuwa sehemu ya Brigade 201 iliyokuwa ikifanya mazoezi Arusha kabla ya kutangazwa rasmi kwa Vita ya Kagera na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Mary alisema kutokana na umuhimu wa mawasiliano wakati huo, aliendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutumia mfumo wa redio, akifanya kazi kuanzia Mutukula hadi ndani ya Uganda kabla ya kurejeshwa nyuma kutokana na mazingira ya operesheni na kuwa mwanamke pekee katika eneo hilo.
“Ukiizingatia wakati ule mawasiliano ilikuwa ni njia ya redio pekee yake, ilikuwa hakuna mawasiliano mengine. Baadaye tukasogea mpaka Mutukula na kisha kuvuka Mutukula pande wa Uganda,” alisema.
Baada ya ushindi wa vita, alisema aliendelea kufanya kazi nchini Uganda katika Ikulu ya Entebbe kuanzia mwaka 1979 hadi 1980 wakati Tanzania ikiendelea kusaidia kurejesha utulivu nchini humo.
Alikumbuka mapokezi makubwa yaliyofanyika Bwananyanja Julai 15, 1979 ambapo Baba wa Taifa na Amiri Jeshi Mkuu wa wakati huo, Mwalimu Nyerere aliwapokea wanajeshi waliorejea kutoka vitani huku Watanzania wakisherehekea ushindi huo kwa furaha kubwa.
Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa huadhimishwa kila mwaka Julai 25 kwa lengo la kuwakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliotoa mchango mkubwa katika historia ya Tanzania hususani katika harakati za kupigania uhuru, kulinda mipaka ya nchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Sherehe hizo za kitaifa zilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa serikali wakiwemo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba. Pia walikuwapo viongozi wa dini, mabalozi na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Aidha Sherehe hizo zilipambwa na gwaride la heshima lililopiga ala ya ‘Last Post’ huku wanajeshi wakishusha silaha zao kwa ishara ya maombolezo. Aidha, mizinga miwili ilifyatuliwa na taifa likasimama kimya kwa dakika moja kuwakumbuka mashujaa wote waliopoteza maisha wakitumikia taifa.
Baada ya kupokea salamu ya heshima ya Rais kutoka kwa gwaride, Rais Samia aliweka mkuki na ngao kwenye mnara huo. Rais Samia alifuatiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, aliyeweka sime, huku Kiongozi wa mabalozi nchini, Balozi wa Burundi, Leontine Nzeyimana aliweka shada la maua kuwakumbuka mashujaa hao.
Viongozi wa dini pia waliongoza sala na dua maalumu kuwaombea mashujaa waliopoteza maisha, huku wakiiombea Tanzania iendelee kudumisha amani, umoja, mshikamano na maendeleo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464