Wananchi wa Mkoa wa Iringa wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Utalii Kihesa, mjini Iringa, ili kujifunza teknolojia za kisasa za kilimo, mifugo na uvuvi, kupata taarifa za masoko pamoja na kukutana na wadau mbalimbali wanaoweza kuongeza tija na kipato chao.
Maonesho hayo, yanayofanyika kwa mara ya kwanza kwa ngazi ya mkoa, yanatajwa kuwa hatua muhimu ya kusogeza huduma karibu na wakulima, wafugaji na wavuvi, badala ya kulazimika kusafiri umbali mrefu kuhudhuria maonesho ya kanda.
Akifungua maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema Nanenane si jukwaa la maonesho pekee, bali ni darasa la vitendo linalowawezesha wazalishaji kujifunza mbinu mpya za uzalishaji, matumizi ya teknolojia, uchakataji wa mazao na namna ya kupata masoko yenye uhakika.
Alisema maendeleo ya sekta ya kilimo hayawezi kutegemea kuongeza uzalishaji pekee, bali yanahitaji matumizi ya mbegu bora, pembejeo sahihi, teknolojia za kisasa, umwagiliaji, ubunifu, uwekezaji na ushirikiano wa wadau ili kuongeza tija na thamani ya mazao.
Kheri alisema Iringa ni miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kutokana na ardhi yenye rutuba, hali nzuri ya hewa na rasilimali za maji.
Alisema mwaka 2023 mkoa ulizalisha zaidi ya tani milioni moja za mazao ya chakula na tani 137,888 za mazao ya biashara.
Hata hivyo, alisema changamoto bado ipo kwa baadhi ya wakulima kuzalisha bila kuzingatia mahitaji ya soko, jambo linalosababisha kushuka kwa bei na kupunguza faida ya uzalishaji.
Alisisitiza umuhimu wa wakulima kupata taarifa za masoko kabla ya kuanza uzalishaji.
Aidha, aliwataka wananchi kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa sekta ya utalii mkoani Iringa kwa kuzalisha mazao yanayohitajika katika hoteli na maeneo ya utalii, ikiwemo mboga mboga, matunda na mazao mengine yenye thamani kubwa sokoni.
Kwa wakazi wa Manispaa ya Iringa, Mkuu huyo wa Mkoa alihimiza matumizi ya maeneo madogo ya makazi kwa kilimo cha bustani ili kupunguza gharama za maisha na kuongeza kipato cha familia.
Alisema maonesho hayo yataendelea kufanyika kila mwaka, yakianzia Manispaa ya Iringa kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuhamia halmashauri nyingine za mkoa, hatua itakayowezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma hizo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa anayeshughulikia Uchumi na Sekta za Uzalishaji, Elias Luvanda, alisema maonesho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo.
Alisema washiriki 87 wanashiriki maonesho hayo, zikiwemo halmashauri zote za Mkoa wa Iringa, taasisi za utafiti, kampuni za mbegu na pembejeo, taasisi za fedha, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Naye Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, alisema maonesho hayo yatafungua fursa mpya za biashara na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika manispaa hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, alisema teknolojia na maarifa yanayooneshwa katika maonesho hayo yanapaswa kuwafikia wakulima wengi zaidi ili yawe chachu ya kuongeza uzalishaji, kuinua kipato na kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Iringa.
