` MCT YAKUTANISHA VIONGOZI WA VYOMBO VYA HABARI KUJADILI UHURU NA MUSTAKABALI WA TASNIA

WANDAMAN HOTEL

MCT YAKUTANISHA VIONGOZI WA VYOMBO VYA HABARI KUJADILI UHURU NA MUSTAKABALI WA TASNIA

 

Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa Siku Mbili wa Mashauriano kati ya MCT na viongozi wa vyombo vya habari unaofanyika Morogoro Julai 16–17, 2026.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Siku Mbili wa Mashauriano kati ya MCT na viongozi wa vyombo vya habari unaofanyika mkoani Morogoro Julai 16–17, 2026. Mkutano huo unajadili mafanikio, changamoto na mustakabali wa tasnia ya habari nchini katika kipindi cha miaka 30 ya mfumo wa kujisimamia.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, akifungua Mkutano wa Siku Mbili wa Mashauriano kati ya MCT na viongozi wa vyombo vya habari unaofanyika mkoani Morogoro Julai 16–17, 2026.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari, kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari na kusimamia maadili ya wanahabari nchini kwa kipindi cha miaka 30, huku likitoa mchango mkubwa katika kujenga tasnia yenye uwajibikaji na kuaminika nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, wakati akifungua Mkutano wa Siku Mbili wa Mashauriano kati ya MCT na viongozi wa vyombo vya habari unaofanyika Morogoro Julai 16–17, 2026, ambapo amewasilisha tafakuri ya miaka 30 ya mfumo wa kujisimamia kwa sekta ya habari nchini.

Amesema katika kipindi hicho MCT imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha tasnia ya habari, huku pia ikitathmini changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kupendekeza hatua za kujenga mustakabali imara wa uandishi wa habari nchini Tanzania.

“Kwa miaka 30 MCT imeokoa vyombo vya habari kwa usuluhishi nje ya mahakama, imejengea uwezo waandishi wa habari, imefanya uchechemuzi wa sera na sheria mbalimbali zinazohusu tasnia, imeandaa na kusimamia kanuni za maadili ya uandishi wa habari zinazotumika kitaifa na mfumo wa kujisimamia umetambuliwa kimataifa kama mfano wa usimamizi wa kitaaluma,” amesema Sungura.

Hata hivyo, Sungura amebainisha kuwa mafanikio hayo yameambatana na changamoto zinazoendelea kuikabili MCT na sekta ya habari kwa ujumla. 

Ametaja mshikamano wa sekta umedhoofika, uchumi wa vyombo vya habari umedorora na sekta bado inakabiliwa na changamoto za uhuru wa vyombo vya habari, kupungua kwa imani ya umma kwa vyombo vya habari na kuongezeka kwa hofu kuhusu usalama wa wanahabari.

Akizungumzia mustakabali wa sekta hiyo, Sungura amependekeza kuanzishwa kwa mfuko endelevu wa kusaidia vyombo vya habari kiuchumi na kufanyika kwa marekebisho ya sera na sheria ili maamuzi ya MCT yatambuliwe kisheria. 

Aidha, amezitaka taasisi za habari kubuni vyanzo vipya vya mapato kupitia huduma za kidijitali, usajili wa wanachama, matukio maalumu, matangazo na huduma za data, huku akisisitiza umuhimu wa kurejesha imani ya umma kupitia maadili, uwajibikaji na weledi.

Mkutano huo umeandaliwa na MCT kwa kushirikiana na VIKES –ambayo ni taasisi ya Finland ya Vyombo vya Habari na Maendeleo, ukiwakutanisha viongozi 21 wa sekta ya habari, wakiwemo wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari na mameneja wa vyumba vya habari. 

Washiriki wanajadili changamoto zinazoibuka na fursa mpya zinazoathiri mustakabali wa uandishi wa habari nchini.

Mkutano huu unafanyika wakati sekta ya habari ikikabiliwa na kasi ya mabadiliko ya teknolojia za kidijitali, matumizi yanayoongezeka ya akili unde (AI), mabadiliko ya matarajio ya jamii, changamoto za usalama wa wanahabari na hitaji la kuimarisha ubora wa taarifa pamoja na kurejesha imani ya umma kwa vyombo vya habari.

 






Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464