Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, imetoa mbinu mbalimbali inazotumia kukusanya mapato ya ndani na kufikia malengo, kwa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro, ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
TAZAMA VIDEO👇👇
Mbinu hizo zimetolewa leo Julai 16, 2026, wakati wa ziara ya mafunzo iliyoshirikisha wataalamu, wakuu wa idara na baadhi ya madiwani kutoka Halmashauri ya wilaya ya Morogoro, waliotembelea Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Dk. Kalekwa Kasanga, amesema siri ya mafanikio yao katika kasi ya ukusanyaji wa mapato, na kuvuka malengo ya kila mwaka wa fedha, ni kuimarisha vyanzo vilivyopo na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato.
"Katika kuimarisha vyanzo hivi, mimi ndiye msimamizi mkuu, lakini wasimamizi wasaidizi ni wakuu wa idara ambapo kila mmoja ana jukumu la kusimamia chanzo kilicho chini ya idara yake, amesema Dk. Kalekwa.
Amesema, pia wameimarisha timu ya ukusanyaji wa mapato pamoja na kuwawezesha kufika katika maeneo yote ya mapato.
"Kihistoria kwa miaka mitatu mfululizo, makusanyo yetu yamekuwa yakipanda, mwaka wa fedha wa 2023/2024 tulifikia asilimia 101, mwaka 2024/2025 tukafikia asilimia 120, na mwaka uliopita wa 2025/2026 tumefikisha asilimia 120.2.” ameongeza.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Diwani Jesca Joseph, amesema wamekuja kwenye mafunzo ya ukusanyaji wa mapato katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na kwamba wamejifunza mambo mengi namna ya kufanya ubunifu katika ukusanyaji wa mapato na kuongeza mapato ya halmashauri.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Kalekwa Kasanga akizungumza.
Diwani Jesca Joseph akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro.