` WATANZANIA WATAKIWA KUACHANA NA TAARIFA ZISIZO SAHIHI ZA MITANDAO YA KIJAMII KUHUSU UBIA WA TANZANIA NA EU

WANDAMAN HOTEL

WATANZANIA WATAKIWA KUACHANA NA TAARIFA ZISIZO SAHIHI ZA MITANDAO YA KIJAMII KUHUSU UBIA WA TANZANIA NA EU



Watanzania Watakiwa Kutozingatia Taarifa Zisizo Sahihi za Mitandao ya Kijamii Kuhusu Ubia wa Tanzania na EU

Serikali imewataka wananchi kuachana na taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari ambazo zinapotosha ukweli kuhusu kura iliyopigwa na Bunge la Ulaya.

Kupitia taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, imesisitizwa kuwa kura hiyo iliyopigwa Juni 18, 2026, kuhusu Mpango wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) kwa mwaka 2026 si uamuzi wa mwisho wa EU kuhusu programu hiyo yenye thamani ya Euro milioni 156.

Serikali imebainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu tu ya mchakato wa ndani wa taasisi za EU ambapo Bunge limetoa maoni na mapendekezo kwa mamlaka nyingine zinazohusika na maamuzi ya mwisho, na sio tamko la kusitisha ushirikiano.

Kinyume na upotoshaji unaoenea mitandaoni, mapendekezo yaliyotolewa na Bunge la Ulaya hayahusu kusimamishwa kwa fedha za programu zinazotekelezwa au zinazotarajiwa kutekelezwa nchini, bali yanahusu kufanyiwa mapitio kwa programu hiyo na kuwasilishwa tena.

Serikali imefafanua kuwa mapitio yoyote ya programu ya ubia hufanyika kwa njia ya mashauriano na makubaliano ya pande zote mbili na hatimaye kuridhiwa kupitia Mkataba wa Pamoja wa Fedha.

Aidha, imeelezwa kuwa kati ya Euro milioni 156 zilizotengwa, Euro milioni 17 pekee ndizo zilizopangwa kupitia moja kwa moja katika mifumo rasmi ya Serikali, huku kiasi kilichobaki cha takribani Euro milioni 139 kikitarajiwa kutekelezwa kupitia taasisi teule za EU, nchi wanachama, na asasi za kiraia.

Pia, Serikali imebainisha kuwa baadhi ya hoja zilizomo katika azimio hilo hazina uhalisia na haziakisi hatua zinazoendelea kuchukuliwa nchini baada ya matukio ya Oktoba 2025.

Licha ya kwamba Serikali ilitoa ufafanuzi wa kina kwa wabunge wa Bunge la Ulaya kabla ya upigaji kura huo na kusikitishwa na hatua ya kutozingatiwa kwa maelezo hayo, imewahakikishia wananchi kuwa uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya unaendelea kubaki imara na thabiti.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464