` CHADEMA SHINYANGA YAPATA VIONGOZI WAPYA

WANDAMAN HOTEL

CHADEMA SHINYANGA YAPATA VIONGOZI WAPYA


Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga, kimefanya uchaguzi wa ndani kwa ajili ya kupata viongozi wapya wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi, baada ya baadhi ya viongozi wake kuhamia vyama vingine.

Uchaguzi huo umefanyika leo, Juni 15, 2026, mjini Shinyanga.
Akizungumza wakati wa uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chadema Kanda ya Serengeti Maendeleo Makoye, amesema uchaguzi huo umefanyika ili kuziba nafasi za viongozi waliohama ili kuhakikisha kazi ya ujenzi wa chama inaendelea.

Ametaja nafasi zilizokuwa zikigombewa kuwa ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa, Katibu wa Baraza la Wanawake Mkoa, pamoja na Mwenyekiti na Katibu wa Baraza la Vijana.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Makoye amesema wajumbe waliotarajiwa kushiriki walikuwa 68, lakini waliohudhuria ni 61 na wote walipiga kura, huku kura moja ikiharibika.

Amemtangaza Peter Machanga, kuwa ndiye aliyeibuka mshindi katika nafasi ya Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga kwa kupata kura 35 sawa na asilinia 57, dhidi ya Mgombea mwenzake Frank Joshua aliyepata kura 25 sawa na asilimia 40.98.
Pia, amewatangaza wagombea wengine, kuwa nafasi ya Baraza la Wazee (BAZESHA) Mkoa, Mwenyekiti ni Willson Mjinja, Katibu (BAWACHA) Mkoa Zena Gulam, na Mwenyekiti (BAVICHA) Joseph Kulagwa na Katibu wake Fungameza Mhoja.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Mwenyekiti mpya wa Chadema Mkoa wa Shinyanga Peter Machanga, amesema chama hicho kwa sasa kipo katika mikono salama, huku akiahidi kuunganisha wanachama na kuondoa migogoro iliyopo ndani ya majimbo ili chama kiwe na umoja.
Awali, Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti Jackson Mnyawami, amesema kwa kipindi cha miaka miwili chama hicho kilikosa msemaji katika ngazi ya mkoa, na aliwataka wajumbe hao kufanya uchaguzi huru na haki, ili kupata viongozi sahihi watakaokipigania chama.

MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti Jackson Mnyawami akizungumza.
simamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chadema Kanda ya Serengeti Maendeleo Makoye akitangaza wagombea.
Mwenyekiti mpya wa Chadema Mkoa wa Shinyanga Peter Machanga akizungumza.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464