Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Ndege ya majaribio imefanikiwa kutua na kuruka katika Uwanja wa Ndege wa Shinyanga leo Juni 12, 2026, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuanza kwa huduma rasmi za usafiri wa anga kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo jirani.
TAZAMA VIDEO👇👇
Baada ya majaribio hayo yaliyohusisha ndege iliyowasili kutoka Uwanja wa Ndege wa Musoma baada ya hapo iliruka kuelekea Dodoma.
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, akizungumza kwenye hafla hiyo, ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo unakamilika kwa asilimia 100 ifikapo Septemba 1 mwaka huu ,ili ndege za abiria zianze kutua na kutoa huduma.
Profesa Mbarawa amesema anaufahamu mradi huo tangu ulipoanza kutekelezwa alipokuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, akisisitiza kuwa ni lazima ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Amesema viwanja vya ndege vya Tabora, Sumbawanga na Kigoma tayari vimekamilika, hivyo hakuna sababu ya Uwanja wa Ndege wa Shinyanga kuchelewa kukamilika.
Aidha, amesema ujenzi wa uwanja huo pamoja na miradi mingine ya viwanja vya ndege nchini unalenga kuimarisha mtandao wa usafiri wa anga, kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji pamoja na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema kukamilika kwa uwanja huo kutakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa mkoa kwa kuwezesha usafiri wa haraka wa watu na mizigo pamoja na kuvutia wawekezaji.
Naye Mkurugenzi wa Miradi wa TANROADS Mhandisi Japherson Nnko, amesema mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga ulianza Aprili 2023 na ulipitia changamoto zilizochelewesha utekelezaji wake kwa muda.
Amesema mradi huo wenye thamani ya Sh. bilioni 45 sasa umefikia asilimia 98 ya utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 30, 2026, tayari kwa kuanza kutoa huduma za ndege za abiria kuanzia Septemba 1 mwaka huu.
MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Waziri wa Uchukuzi Prof Makame Mbarawa akizungumza.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.
Naye Mkurugenzi wa Miradi wa TANROADS Mhandisi Japherson Nnko akizungumza.
Ndege ikiwasili uwanja wa ndege Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464