` BALOZI MATINYI AKABIDHI HATI KWA RAIS WA ALGERIA

WANDAMAN HOTEL

BALOZI MATINYI AKABIDHI HATI KWA RAIS WA ALGERIA

  

Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi akisalimiana na Mheshimiwa Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, mara baada ya kukabidhi hati za utambulisho wa kibalozi katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Algiers tarehe 10 Juni, 2026. Katikati ni Mheshimiwa Ahmed Attaf, Waziri wa Mambo wa Nje wa Algeria.
Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi akizungumza na waandishi wa habari wa Algeria mara baada ya kukabidhi hati zake za utambulisho wa kibalozi kwa Mheshimiwa Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Algiers tarehe 10 Juni, 2026. Kushoto kwake ni Mwambata wa Ulinzi Kanali Nassoro Kapolo na kushoto kwake ni Afisa wa Ubalozi, Maryam Kilongo.

***

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare  Matinyi, amekabidhi hati za utambulisho wa kibalozi kwa Mhe. Rais Abdelmadjid Tebboune wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya jijini Algiers, tarehe 10 Juni, 2026, ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi utekelezaji wa majukumu ya kibalozi.

Katika mazungumzo yao mafupi yaliyofuatia baada ya hafla hiyo, Mhe. Balozi Matinyi alimshukuru Mhe. Rais Tebboune, serikali na watu wa Algeria kwa niaba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kudumisha ushirikiano wa kindugu wa nchi hizi mbili ambao umedumu kwa zaidi ya miongo sita.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya mazungumzo yake na Mhe. Rais Tebboune, Balozi Matinyi alisema kwamba walijadiliana namna ya kusonga mbele baada ya kufikia mafanikio mazuri katika sekta za ulinzi na elimu ya juu ili kuhakikisha watu wa nchi hizi wananufaika pia katika sekta zingine muhimu.

Mhe. Balozi Matinyi alizitaja sekta walizojadiliana kwamba zinahitaji kufanyiwa kazi hivi sasa kuwa ni kilimo, viwanda, utengenezaji dawa, nishati, madini na utalii pamoja na kuongeza ushirikiano katika sekta za ulinzi, elimu ya juu, sayansi, teknolojia, utafiti na utamaduni ili kuboresha ushirikiano baina ya watu wa nchi zote mbili.

“Nimepewa jukumu na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba ushirikiano wa nchi hizi mbili unawanufaisha watu wa mataifa yetu mawili na kwa kutumia umahiri wa marais wetu tutafanikiwa,” alisema Mhe. Balozi Matinyi alipozungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya Algiers baada ya hafla hiyo.

Aidha, Mhe. Rais Tebboune alisema wakati wa mazungumzo yao kwamba Algeria iko tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta zote muhimu na itakuwa tayari kufikia makubaliano ya ushirikiano zaidi kupitia vikao vya pamoja na ziara za viongozi kama alivyopendekeza Mhe. Balozi Matinyi.

Mhe. Balozi Matinyi anakuwa balozi wa nne kuiwakilisha Tanzania nchini Algeria baada ya Mhe. Balozi Omari Yussuf Mzee (2017-2020), Mhe. Balozi Meja Jenerali Jacob Kingu (2020-2023) na Mhe. Balozi Imani Njalikai (2023-2026). Ubalozi wa Algiers huiwakilisha pia Tanzania katika nchi za Tunisia, Mauritania, Niger na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi (SADR).

Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania,

Algiers, Juni 10, 2026.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464