` UNODC YAPONGEZA TANZANIA KWA KULINDA AMANI YANOA POLISI KUKABILIANA NA UHALIFU

WANDAMAN HOTEL

UNODC YAPONGEZA TANZANIA KWA KULINDA AMANI YANOA POLISI KUKABILIANA NA UHALIFU

Tanzania imepongezwa kwa kuendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye usalama, amani na utulivu katika Bara la Afrika licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za uhalifu wa kimataifa.

Pongezi hizo zimetolewa jana jijini Mwanza na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Andres Reyes kutoka Colombia, wakati akifunga mafunzo maalumu ya wiki nne kwa Polisi Wanamaji kuhusu kuzuia, kukagua na kukamata vyombo vya majini.

Katika hotuba yake aliupongeza mkoa wa Mwanza na viongozi wa nchi kwa ujumla kwa jitihada hizo za kulinda amani. 

Reyes alieleza kuwa kutokana na mazingira hayo tulivu, UNODC itaendelea kutoa mafunzo maalumu kwa Polisi Wanamaji pamoja na vikosi vingine vya usalama ili kuimarisha uwezo wa kupambana na uhalifu katika maeneo ya majini, akibainisha kuwa ushirikiano uliopo umeleta mafanikio makubwa katika kukabiliana na changamoto hizo. 

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo askari kukabiliana na vitendo vya magendo, uvuvi haramu, usafirishaji wa silaha haramu, na aina nyingine za uhalifu wa majini kupitia mbinu za nadharia na vitendo zitakazosaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuimarisha usalama wa mipaka ya maji na nchi kavu. 

Reyes aliongeza kuwa hiyo ni mara yake ya tatu kutembelea Mkoa wa Mwanza na amefurahishwa mno na ushirikiano anaoupata kutoka kwa viongozi wa serikali pamoja na Jeshi la Polisi katika utoaji wa elimu na mafunzo hayo.

Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Florence Mwenda alisema Jeshi la Polisi mkoani humo litaendelea kuwajengea uwezo askari wake kupitia mafunzo ya ndani na nje ya nchi ili kukabiliana na wahalifu ambao wamekuwa wakibadili mbinu zao kutokana na maendeleo ya teknolojia na utandawazi. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464