` KILIMANJARO MFANO WA MISINGI YA AMANI ILIYOWEKWA NA WATANGULIZI

WANDAMAN HOTEL

KILIMANJARO MFANO WA MISINGI YA AMANI ILIYOWEKWA NA WATANGULIZI

Tathmini ya kina ya siasa na mwelekeo wa sasa wa taifa inalazimu Watanzania kutazama nyuma kwa umakini ili kujifunza na kutokubali kurudishwa kabisa katika ghasia na vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa matukio ya Oktoba 29.

 Wakati wa ghasia hizo zilizotishia utulivu wa nchi, Mkoa wa Kilimanjaro ulionyesha ukomavu mkubwa kwa kutulia na kubeba historia yake vyema, ukiendelea kusimama kama mfano bora wa eneo linalokataa ushawishi hasi unaoweza kubomoa mustakabali wa nchi.

Sifa kuu ya mkoa huo imekuwa ni kutoa viongozi mashuhuri, wenye uzoefu, na maono makubwa ya mbele waliolitumikia taifa hili kwa nyakati tofauti na kusimamia maendeleo yake kwa weledi.

Katika muktadha huu, kuna umuhimu mkubwa kwa Watanzania kwa sasa kutokubali kurubuniwa na watu wanaotaka kuharibu misingi imara ya amani, umoja, na mshikamano iliyoasisiwa na viongozi wetu wenye maono waliotutangulia. 

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, akiwa katika ziara mkoani Kilimanjaro, amesisitiza kuwa uongozi wa taifa si jambo la majaribio, na hivyo nchi haipaswi kukabidhiwa kwa watu wasio na "leseni" ya uongozi au wasioelewa historia na mahitaji ya wananchi. 

Amesema ni wajibu wa kila mwananchi kulinda tunu hizi muhimu za kitaifa kwa sababu ndizo zinazoweka mazingira salama ya kupiga hatua mbele.

Uthabiti wa amani na utulivu wa kisiasa unatoa nafasi ya moja kwa moja kwa serikali kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake bila usumbufu. 

Ushahidi wa faida za amani unaonekana wazi mkoani Kilimanjaro kupitia ukaguzi wa mradi wa kimkakati wa mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, uliogharimu shilingi bilioni 1.94 chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.

 Mradi huo uliowezesha kuzalishwa kwa mitungi 3,313 ya oksijeni na kuokoa shilingi milioni 126 ndani ya miezi sita, ni kielelezo tosha kwamba nchi inapokuwa tulivu na wananchi wanapokataa rubuni za kisiasa, rasilimali na nguvu za taifa huelekezwa kwenye kuboresha miundombinu ya matibabu na kuokoa maisha ya jamii.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464