
Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ability Sweli, ambaye anaishi nchini Tanzania kwa shughuli za utafutaji maisha, ametoa onyo kali kwa Watanzania wanaotumia mitandao ya kijamii kuchochea uvunjifu wa amani, akieleza kuwa vitendo hivyo ni vya kijinga na vinaweza kuliingiza taifa katika majanga makubwa.
Sweli ametoa kauli hiyo kufuatia kuongezeka kwa mahimizano ya vurugu yanayofanywa na baadhi ya watu mtandaoni, akisisitiza kuwa yeye ni mwathirika wa moja kwa moja wa vita nchini kwake na ameshuhudia kwa macho yake namna machafuko yanavyoweza kuporomosha maisha ya mtu mmoja mmoja na uchumi wa nchi kwa ujumla ndani ya muda mfupi.
Akizungumzia uzoefu wake wa kuishi kwenye mazingira ya kivita nchini Kongo, Sweli amebainisha kuwa vita si jambo la kusimuliwa wala kufanyiwa majaribio, kwani huondoa hali ya utulivu na kusitisha maendeleo yote ya kijamii na kiuchumi.
Ameeleza kuwa mnyororo wa maendeleo unategemea amani, na kwamba pasipo amani hakuna mwananchi anayeweza kufanya shughuli zake kwa uhuru wala kupanga mipango ya baadaye.
Sweli ametolea mfano wa Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, akisema kuwa soko hilo limekuwa kivutio cha wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali kutokana na utulivu uliopo nchini, jambo ambalo amedai kuwa ni nadra kuliona katika maeneo yenye migogoro nchini kwake DRC.
Mwathirika huyo amefafanua kuwa wengi wa wanaohamasisha vurugu na kuvunja amani mitandaoni hufanya hivyo kwa sababu hawajawahi kuishi kwenye mazingira ya vita, hivyo hawawezi kutambua thamani ya neema waliyonayo kwa sasa.
Ameonya kuwa siku ambayo vita itatokea na kuwalazimu kuishi ndani ya milio ya risasi, ndipo watakapogundua kwanini kuna umuhimu wa kuhimiza amani kila siku na kwanini sauti za wanaopigania utulivu zinapaswa kuheshimiwa.
Kwa mujibu wa Sweli, faida ya amani huonekana zaidi baada ya watu kupoteza kila kitu kutokana na vita, hali ambayo amewaomba Watanzania wasiiruhusu iwafikie kwa kufuata ushauri wa kijinga unaosambazwa katika majukwaa ya kidijitali.
Aidha, amewataka wananchi kuzingatia amani waliyonayo kama kipaumbele namba moja, akisisitiza kuwa uhuru wa kufanya biashara, kutembea na kujenga nchi unategemea usalama wa mipaka na mioyo ya watu.
Sweli ambaye anaishi nchini kwa mujibu wa taratibu na sheria za uhamiaji, amesema kuwa uzoefu wake wa kuporomoka kimaisha wakati wa vita nchini mwaka unatosha kuwa fundisho kwa yeyote anayedhani kuwa vita ni suluhisho la changamoto za kijamii.
Amesisitiza kuwa ni wakati wa Watanzania kupuuza kila aina ya uchochezi wa mtandaoni na badala yake waendelee kuilinda tunu ya amani ambayo ndiyo siri ya maendeleo makubwa ya kiundombinu na kibiashara yanayoonekana nchini kwa sasa
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464