Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Royal Yawa Mkombozi wa Huduma za Afya Kanda ya Ziwa*
Mwandishi wetu, Mwanza
Wakazi wa Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa wanatarajiwa kunufaika zaidi na huduma za afya kufuatia kufunguliwa rasmi kwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Royal iliyopo Jijini Mwanza.
Mgeni Rasmi Rev.Dr Barnabas Mtokambali akikata utepe.
Uzinduzi wa hospitali hiyo ulifanyika jana ambapo mgeni rasmi alikuwa Askofu Mkuu wa TAG, Rev. Dr. Barnabas Mtokambali, aliyesema kuwa uwepo wa hospitali hiyo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa pamoja na nchi jirani za Maziwa Makuu.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Askofu Mtokambali alisema hospitali hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kibingwa.
Alisema kufunguliwa kwa hospitali hiyo ni fursa kubwa kwa wakazi wa Mwanza na maeneo ya jirani kupata huduma bora za afya karibu na makazi yao.
Aidha, aliwataka wananchi kuitunza miundombinu ya hospitali hiyo ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha miundombinu hii inalindwa na kutunzwa ili iweze kuwahudumia wananchi kwa miaka mingi ijayo,” alisema Rev. Dr. Mtokambali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Royal, Daktari Glory Simon, alisema hospitali hiyo ilianza mwaka 2020 ikiwa katika ngazi ya hospitali ya wilaya na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 70 kwa siku.
Alieleza kuwa kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika, hospitali hiyo sasa imepandishwa hadhi kuwa hospitali ya rufaa ya kanda yenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 200 kwa siku.
“Tumewaita hapa si kwa ajili ya kuona jengo hili pekee, bali kushuhudia kusogezwa kwa huduma muhimu za afya kwa wananchi kupitia maono yetu ya muda mrefu,” alisema Daktari Simon.
Aliongeza kuwa hospitali hiyo inalenga kutoa huduma za kibingwa kwa viwango vya juu ili kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda mikoa mingine au nje ya nchi.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Royal inatajwa kuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Mwanza, Kanda ya Ziwa na nchi za Maziwa Makuu kutokana na kusogeza karibu huduma za kibingwa ambazo awali zilikuwa zinapatikana kwa ugumu mkubwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464



