Watanzania wametakiwa kujadili kwa kuweka mbele maslahi ya taifa Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na Kituo cha Utangazaji cha Uhai jijini Dar es Salaam, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Said Miraji alisema ripoti hiyo ni ajenda ya kitaifa na si mali ya kundi au chama chochote cha siasa.
Alisisitiza kuwa masuala yaliyobainishwa, mapendekezo yaliyotolewa na tume ikiwemo uwajibikaji, usawa na haki yanawahusu Watanzania wote, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuyajadili kwa lengo la kujenga taifa imara.
“Ni muhimu tukakaa na kuangalia mapendekezo yaliyotolewa yana manufaa gani kwa wananchi, kwa pamoja tuyafanye kuwa ajenda ya kitaifa,” alisema Miraji.
Aliongeza kuwa hata wale wasiokubaliana na uundwaji wa tume hiyo wanapaswa kuzingatia yaliyomo kwenye ripoti kwa kuwa yanagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, Dk Faraja Kristomus alisema ripoti hiyo imeibua masuala mengi yaliyowakera hata wananchi wasiokuwa na itikadi za vyama vya siasa wakati na baada ya uchaguzi huo.
Alisisitiza kuwa mchakato wa kufikia muafaka wa kitaifa haupaswi kuachwa mikononi mwa vyama vya siasa pekee, bali unahitaji ushiriki mpana wa wananchi wote.
Aidha, Dk Kristomus alibainisha kuwa katika safari ya kufikia maridhiano ya kitaifa, ni muhimu wananchi kushiriki kikamilifu katika majadiliano ili kuhakikisha ajenda zinazojadiliwa zinanufaisha taifa zima, badala ya makundi maalumu.
Alionya dhidi ya hali ambapo kundi fulani linaweza kujiona lina mamlaka ya kumiliki mifumo ya utawala, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya uraia na uzalendo ili wananchi watambue haki zao na kuwawajibisha viongozi.
Akizungumzia matukio ya uchaguzi huo, alisema yalikuwa ni matokeo ya matatizo yaliyokuwa yakipuuzwa kwa muda mrefu.“Yaliyotokea Oktoba 29 yalikuwa kama bomu lililopasuka baada ya kukaa muda mrefu bila kuteguliwa,” alisema Dkt. Kristomus.
Aliwahimiza Watanzania kujifunza kutokana na yaliyotokea na kuchukua hatua za kutekeleza makubaliano yatakayofikiwa ili kuepusha migogoro isiyo na tija siku zijazo.
