` RAFIKI SDO YASUKUMA AJENDA YA CHAKULA SHULENI

WANDAMAN HOTEL

RAFIKI SDO YASUKUMA AJENDA YA CHAKULA SHULENI

 

RAFIKI SDO YASUKUMA AJENDA YA CHAKULA SHULENI

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

SHIRIKA la Rafiki SDO, limeendelea kuhamasisha utoaji wa chakula shuleni, katika shule zilizopo Kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga, likieleza kuwa mpango huo ni miongoni mwa mikakati muhimu ya kuinua ufaulu wa wanafunzi.

Akizungumza jana wakati wa ziara ya mafunzo kwa wadau wa elimu kutoka Kata ya Kitangili, Mkurugenzi wa shirika hilo Gerald Ng’ong’a, ambao ndiyo wameratibu ziara hiyo, amesema lengo ni kuhakikisha shule zote za Kitangili ikiwamo Iwelyangula, zinaanzisha mpango wa chakula ili kuboresha mazingira ya ujifunzaji.
Ng’ong’a amesema, uzoefu unaonyesha kuwa wanafunzi wanaopata chakula shuleni, huwa na umakini darasani, huhudhuria masomo kikamilifu na kufanya vizuri kwenye mitihani, ndiyo maana wameratibu ziara hiyo, ili wadau hao wajifunze kwa shule ambao zinafanya vizuri mpango wa utoaji wa chakula shuleni.

“Tunataka kuona shule zote katika Kata ya Kitangili ikiwamo Iwelyangula, zinaanzisha mpango huu wa utoaji wa chakula shuleni, kwa sababu lishe bora ni msingi wa ufaulu wa mwanafunzi,” amesema Ng’ong’a.
Mmoja wa wazazi walioshiriki ziara hiyo Mwanne Ngassa kutoa Iwelyangula, amesema, mafunzo hayo yamewabadilisha mtazamo, na sasa wako tayari kushiriki kikamilifu katika uchangiaji wa chakula shuleni.

“Tumeelewa umuhimu wa chakula shuleni, mtoto akila vizuri anakuwa makini darasani, tutakuwa mabalozi wazuri kwa wazazi wenzetu ili tuchangie chakula shuleni,” amesema Mwanne.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Kitangili Fanta Mwendapole, amesema katika shule hiyo hawafanyi vizuri katika utoaji wa chakula,na kusababisha ufaulu wa wanafunzi kuendelea kushuka,na kwamba wamejifunza kitu kuwa shule ambao zinatoa chakula wameendelea kufanya vizuri kitaaluma.

“katika ziara hii tumegundua, ufaulu mzuri ni pale mwanafunzi anaposoma akiwa ameshiba, na ili mwanafunzi afeli, asome akiwa na njaa,” amesema Mwendapole.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Town Meshack Herman, amesema siri ya mafanikio ya shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma, ni utoaji wa chakula shuleni, na hata kuongeza muda wa ziada wa masomo, sababu wanafunzi wanakuwa wameshiba.

Amebainisha kuwa, wao walifanikiwa mpango huo wa utoaji wa chakula shuleni, mara baada ya kufanya vikao na wazazi, na kuwapatia elimu juu mahusiano ya chakula na taaluma ya mtoto.
Amesema, baada ya elimu hiyo, ndipo wazazi walianza kuchangia chakula shuleni, na wale ambao hawakutoa ushirikiano ,walikuwa wakiwaita mmoja mmoja na kuwaonyesha matokeo ya mtoto wake, ambaye hali chakula shuleni na ambaye anakula, jinsi alivyofanya vizuri kuliko mtoto wake.

“katika shule hii ya Msingi Town utoaji wa chakula shuleni ni asilimia 95, na wale ambao wazazi wao hawana uwezo kabisa, sababu watoto wengine wanaishi na Bibi zao wapo kama 50 hivi, wenyewe wanakula bure, ili tuendelee kuwainua kitaaluma ,” amesema Herman.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lubaga, Willelmina Mutayoba, amesema mpango wa chakula shuleni, umechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa zinazofanya vizuri kitaaluma katika manispaa hiyo.

Baadhi ya wanafunzi, akiwemo Fatuma Zuberi, wamesema wanapopata chakula shuleni huweza kuelewa vizuri masomo kutokana na kutokuwa na njaa.

Ziara hiyo imewakutanisha kamati za shule Kata ya Kitangili kwa shule ya Msingi Iwelyangula na Kitangili, viongozi wa serikali za mitaa, walimu, maafisa maendeleo, watendaji wa kata, madiwani pamoja na wazazi, ili wajifunze kwa vitendo kutoka shule zinazotekeleza mpango huo wa chakula kwa mafanikio.

Katika ziara hiyo, washiriki walitembelea Shule za Msingi Lubaga na Town, ambazo zimefanikiwa kutoa chakula kwa wanafunzi na kuongeza kiwango cha ufaulu kitaaluma.

TAZAMA VIDEO KWA CHINI YA PICHA👇👇
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO Gerald Ng'ong'a akizungumza.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Town Meshack Herman akizungumza.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lubaga, Willelmina Mutayoba akizungumza.
Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Lugaba Josephat Nthabind akizungumza.
Diwani wa Vitimaalum Kitangili Moshi Kanji akizungumza.


TAZAMA VIDEO KWA CHINI👇👇
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464