
Wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wameendelea kutoa wito kwa Watanzania kuzingatia utulivu na mshikamano wa kitaifa wakati Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, ikiendelea na kazi yake ya kukusanya maoni na ushahidi.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti katika mahojiano, wananchi hao wameeleza kuwa mchakato huo ni
hatua muhimu ya kujenga maridhiano ya kweli na kurejesha imani miongoni mwa
jamii, wakisisitiza kuwa mafanikio ya tume yanategemea ushirikiano wa wananchi
wote.
Chibura Makorongo
mkazi wa Manispaa hiyo, amesema kuundwa kwa tume hiyo kunaashiria nia ya dhati
ya viongozi wa nchi kusikiliza kilio cha wananchi na kushughulikia changamoto
zilizojitokeza kwa uwazi na haki.
Kwa mujibu wa Makorongo, historia ya Tanzania
kama taifa lenye amani inapaswa kulindwa kwa vitendo, akieleza kuwa juhudi za
kusikiliza pande zote kupitia tume ni njia mojawapo ya kudumisha heshima hiyo
ndani na nje ya nchi.
Naye mkazi mwingine
Peter Omari amesema mazungumzo ya wazi
ndiyo msingi wa suluhu ya kudumu, akibainisha kuwa kila mwananchi anapaswa
kutumia fursa hiyo kueleza yaliyompata ili kusaidia kupatikana kwa ukweli.
Akichangia hoja hiyo, Joramu Mihayo wa eneo
la Kambarage amesema kuwa mshikamano wa kitaifa unahitaji moyo wa kuvumiliana
na kusameheana badala ya kutumia nguvu.
Kwa upande wake Pendo Herman mkazi wa Mtaa wa Ngokolo amesema hatua ya serikali
kuunda tume hiyo imeleta matumaini mapya kwa wananchi, hususan wale walioguswa na
matukio hayo ambapo amesema kila Mtanzania anapaswa kutambua kuwa amani ni
nguzo kuu ya maendeleo, hivyo inapaswa kulindwa kwa vitendo kupitia ushiriki
katika mchakato wa maridhiano.