
Afisa usafirishaji wa bodaboda, Shabani Adam, mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kulinda na kuthamini amani iliyopo nchini, akieleza kuwa hatamani kuona hali ya utulivu ikitoweka kwa namna yoyote ile.
Akizungumza kwa
hisia, Shabani amesema kuwa amani ni nguzo muhimu ya maisha ya kila siku,
akisisitiza kuwa hakuna furaha ya kweli kwa mtu au jamii endapo hakuna utulivu
wa ndani ya moyo na katika taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa
Watanzania wanapaswa kumshukuru Mungu kwa kuijalia nchi yao hali ya umoja,
mshikamano na amani, ambayo imewawezesha kuishi na kufanya shughuli zao za
kiuchumi bila hofu wala bughudha.
Kwa mujibu wa
Shabani, mchango wa vyombo vya ulinzi na usalama ni mkubwa katika kuhakikisha
wananchi wanaendelea kuishi kwa amani, Amesema majeshi hayo yamekuwa mstari wa
mbele kulinda usalama wa raia na mali zao, jambo linalowafanya wananchi
kujivunia nchi yao.
Aidha, ameiomba
serikali kuendelea kuviimarisha vyombo hivyo ili viweze kutekeleza majukumu yao
kwa ufanisi zaidi, akibainisha kuwa uwekezaji katika usalama wa taifa ni
uwekezaji katika ustawi wa wananchi wake.
Shabani pia
amesisitiza kuwa hatamani kuona vurugu za aina yoyote zinatokea, iwe ni kati ya
wananchi wenyewe, kati ya wananchi na serikali, au hata baina ya mataifa,
akieleza kuwa migogoro huathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo na ustawi wa jamii.
Amehitimisha kwa kusema kuwa uhuru uliopo watanzania
wa kufanya kazi mchana na usiku bila hofu ni jambo la kujivunia, hivyo ni
jukumu la kila mmoja kuhakikisha amani hiyo inadumu milele kwa manufaa ya
kizazi cha sasa na kijacho.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464