` MFUMO MPYA WA KIDJITAL KUTUMIKA KUCHUJA TUZO ZA EJAT 2026

WANDAMAN HOTEL

MFUMO MPYA WA KIDJITAL KUTUMIKA KUCHUJA TUZO ZA EJAT 2026


Na Beda Msimbe

Tuzo za 16 za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) zinatarajiwa kuweka historia mpya kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa kidijitali wa kuchakata kazi za washiriki, ukiwa na lengo la kuongeza uwazi na ufanisi.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari nchini (MCT), Ernest Sungura, ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 13,2026 wakati wa hafla ya kutambulisha na kuapisha majaji 12 watakaosimamia mchakato huo.

Alibainisha kuwa mfumo huo mpya ni matokeo ya utafiti wa miaka miwili, ukilenga kuhakikisha ushindani unakuwa wa gharama nafuu (cost-effective) na wenye ufanisi mkubwa.


Tofauti na miaka ya nyuma, tuzo za mwaka huu zimeweka msisitizo mkubwa kwenye matokeo (impact) ya habari iliyoandaliwa.

"Ushindi hautategemea mfumo pekee; kutakuwa na hatua ya uhakiki ambapo majaji watafika hadi eneo la chanzo cha habari ili kuthibitisha matokeo ya kazi husika kabla ya kutangazwa kwa wateule (nominees) ifikapo Mei 29, 2026," alisema Sungura.

Aidha, mfumo huo utaruhusu wadau na washiriki kuona alama (scores) zilizotolewa na kila jaji, jambo linalolenga kuimarisha uaminifu wa tuzo hizo ambazo huzingatia viwango vya juu vya kitaaluma.

Inaelezwa kuwa takriban waandishi 600 walituma kazi zao, lakini idadi hiyo itapungua baada ya mchakato wa ndani kuondoa kazi ambazo hazikukidhi vigezo vya kitaaluma na kiufundi.


Majaji tisa waliapishwa na Wakili Msomi Ally Kileo kusimamia mchakato wa tuzo hizo huku wengine watatu wakisubiri kuaopishwa baadae.Majaji walioapishwa ni Beatrice Bandawe, Joyce Shebe, Jesse Kwayu, Rashid Kejo, Dk. Egbert Mkoko, Hassan Mheleke, Absalom Kibanda, Neville Meena na Mwanzo Milinga. Majaji watatu Aisha Dachi, Sauli Juliagi na Shifaa Said Hassan hawakuhudhuria hafla hiyo na watatafutiwa muda mwingine wa kuapishwa.


Wakizungumza baada ya kuapishwa, baadhi ya majaji walieleza utayari wao wa kulinda heshima ya taaluma.

Joyce Shebe alieleza shukrani zake kwa kuaminika: "Mimi ni nani kati ya waandishi maelfu waliopo? Nashukuru kwa kuaminika na nitatekeleza kiapo changu kuleta mshindi ambaye kweli anastahili."

Kwa upande wake, Rashid Kejo alisisitiza kuwa nafasi hiyo ni dhamana kubwa na atahakikisha anatenda haki kitaaluma, huku Beatrice Bandawe akisema amehishimishwa kuteuliwa kwa mara ya pili kuwa jaji wa tuzo hizo kubwa nchini.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464