` RIPOTI YA TUME YA JAJI CHANDE YATOA DIRA MPYA YA MARIDHIANO TANZANIA

WANDAMAN HOTEL

RIPOTI YA TUME YA JAJI CHANDE YATOA DIRA MPYA YA MARIDHIANO TANZANIA

Stella Herman, Shinyanga

Ripoti ya Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi  mkuu Octoba 29,2025 iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mohamed Chande  imeelezwa kuleta faraja kubwa kwa watanzania huku ikiashiria mwelekeo wa serikali katika kujenga maridhiano, umoja na kudumisha amani nchini.

Wengi wanaona kuwa yaliyomo ndani ya ripoti hiyo yanaweza kuwa msingi imara wa kuimarisha mshikamano wa kitaifa endapo yatapewa uzito unaostahili hatua ambayo inakwenda kuleta maridhiano na kuendelea kuliunganisha taifa kuwa kitu kimoja.

Akitoa maoni yake mkurugenzi wa Taasisi ya Joseph Muhunda Nyerere Foundation, Chifu  Muhunda  Nyerere amesisitiza umuhimu wa serikali kujikita katika kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo. Ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuonesha dhamira ya dhati ya uongozi katika kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kwa njia ya haki na uwazi.

Aidha, amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuyafanyia kazi mapendekezo ya tume hiyo kwa vitendo ili kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa na wananchi. Amesema utekelezaji huo utakuwa ni hatua muhimu katika kujenga imani kati ya serikali na wananchi.

Amesema tume hiyo ilitumia muda mrefu kukusanya maoni na kufanya uchambuzi wa kina, jambo linaloifanya ripoti hiyo kuwa na uzito mkubwa kama dira ya taifa katika kuelekea maridhiano ya kweli.

 Kupitia mapendekezo hayo, Tanzania inaweza kuendelea kuwa mfano wa nchi yenye utulivu na mshikamano ,huku akiwaomba watanzania  kuendelea kuwa kitu kimoja na kushikamana bila kupinga mambo yenye manufaa kwa taifa kwani  maendeleo ya nchi yanategemea umoja wa wananchi wake, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kulinda na kuendeleza amani iliyopo.

Amebainisha kuwa hakuna kiongozi mwenye nia mbaya kwa wananchi, bali dhamira ya serikali ni kuwaletea maendeleo na ustawi. Hivyo, ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuipenda nchi yao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo badala ya kuvuruga misingi ya amani.

Ametoa wito kwa vijana  kuwa makini na kuepuka mihemuko inayoweza kuhatarisha utulivu wa nchi,na kutambua thamani ya Tanzania na kutodanganyika kuwa kuna nchi bora zaidi kuliko yao.

Amewasihi kuipenda, kuitunza na kuwa wazalendo, wakielezwa kuwa kuharibu nchi ni rahisi lakini kuijenga upya ni kazi ngumu inayohitaji muda na juhudi kubwa.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464