
Katika kuimarisha usalama na kukabiliana na vitendo vya uhalifu, Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limefanikiwa kuwakamata watu 63 wanaotuhumiwa kujihusisha na makosa mbalimbali, kufuatia operesheni maalum iliyofanyika kwa mwezi mzima wa Aprili mwaka huu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Aprili 28,2026 amesema operesheni hiyo imefanyika katika kwa lengo la kubaini na kuzuia vitendo vya kihalifu vinavyoathiri usalama wa wananchi.
Amesema miongoni mwa makosa yaliyobainika ni pamoja na wizi wa mafuta ya dizeli lita 295, kukutwa na mifuko 13 ya mawe yanayodhaniwa kuwa ya madini, pamoja na umiliki wa noti bandia zenye thamani ya Sh81,000.
Aidha, katika operesheni hiyo polisi walikamata vielelezo mbalimbali ikiwemo pikipiki 14, simu za mkononi 98, betri za simu 86, bangi gramu 1,100, mirungi kilogramu 103, pombe haramu aina ya moshi (gongo) lita 55 na vipande 21 vya chuma vinavyodhaniwa kuwa vya wizi.
“Operesheni hii imefanyika kwa muda wa mwezi mmoja na tumefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 63 pamoja na vielelezo. Lengo letu ni kuhakikisha tunadhibiti na kuzuia uhalifu katika maeneo yetu,” amesema Magomi.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limebaini jumla ya makosa 4,260 ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani, ambapo wahusika wamechukuliwa hatua za kisheria. Kati ya makosa hayo, magari yalihusika katika makosa 3,030 huku bajaji na pikipiki zikichangia makosa 1,230.
Kamanda Magomi amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu vitendo vya uhalifu, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kudumisha amani na usalama wa jamii.
