Hayo yalisemwa Alhamisi, Aprili 16, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakati akiwasilisha bungeni, jijini Dodoma, mapendekezo ya bajeti ya wizara yake ya Sh144.85 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Prof. Mkumbo alisema Muswada huo unalenga kuweka mfumo mpya wa kisheria wa usimamizi wa uwekezaji wa umma, utakaosaidia kuongeza ufanisi, uwajibikaji na mchango wa mashirika ya umma katika uchumi wa taifa.
Alifafanua kuwa, pamoja na mambo mengine, Muswada huo utapendekeza kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma itakayoratibu na kusimamia uwekezaji wa Serikali kupitia taasisi zake kwa mtazamo wa kitaifa.
Aidha, utapendekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma utakaosaidia upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya uwekezaji kupitia mashirika ya umma, bila kuhatarisha vyanzo vya msingi vya mapato vinavyoingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Katika eneo la uongozi na utawala, Muswada huo utaweka mfumo wa ushindani katika upatikanaji wa Watendaji Wakuu na Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi za mashirika ya umma, hatua inayolenga kuongeza weledi, uwajibikaji na ufanisi katika uendeshaji wa taasisi hizo.
Pia, serikali inalenga kuongeza uhuru wa kiutendaji kwa mashirika ya umma yanayofanya biashara, ili kuyawezesha kujiendesha kwa tija zaidi, kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali na kuimarisha ushindani katika sekta zake.
Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya mashirika na kampuni 308 zikiwemo zile ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache zenye thamani ya uwekezaji ya Sh92.3 trilioni ambapo kati yake 91 ni mashirika ya kibiashara.
Hata hivyo, Prof. Mkumbo alisisitiza kuwa uhuru kwa mashirika hayo utaambatana na mifumo madhubuti ya upimaji utendaji ili kuhakikisha mashirika hayo yanabaki kuwajibika na kutoa matokeo yanayotarajiwa.
Katika mwaka wa fedha 2026/27, Serikali pia itaendelea na zoezi la tathmini ya kina ya utendaji wa mashirika na taasisi za umma, ambapo itachukua hatua stahiki ikiwemo kuunganisha taasisi na mashirika yenye majukumu yanayofanana, kufuta yale ambayo malengo yake yamepitwa na wakati au majukumu yake yanaweza kutekelezwa na taasisi nyingine, pamoja na kuboresha yale yenye changamoto za kiutendaji.
Kufuatia tathmini ya utendaji na majukumu ya mashirika ya umma iliyofanyika mwaka 2023, Serikali ilielekeza kuunganishwa kwa mashirika ya umma 14 na kufutwa kwa mashirika mengine matatu.
Hadi sasa, mashirika matatu yameshafutwa na mengine mawili yameunganishwa, ambapo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) ziliunganishwa na kuunda Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA).
Prof Mkumbo alisema Serikali inaendelea na kukamilisha taratibu za kisheria kuunganisha mashirika yaliyobaki.
Aidha, alisema kwa mwaka wa fedha 2026/27 Ofisi ya Msajili wa Hazina inatarajia kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya Sh1.79 trilioni yatakayochangia Mfuko Mkuu wa Serikali, ikilinganishwa na lengo la Sh1.69 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Akielezea mwenendo wa ukusanyaji kwa mwaka huu wa fedha, alisema hadi Machi 2026 mapato yasiyo ya kodi yamefikia Sh773.37 bilioni, kutoka Sh664.53 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka uliopita, hatua inayoonesha kuimarika kwa utekelezaji wa malengo ya mapato.
Alifafanua kuwa mapato hayo yanatarajiwa kutokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo gawio kutoka taasisi za umma, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ya taasisi, mapato yatokanayo na Mfumo wa Usimamizi wa Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTMS), marejesho ya mikopo na riba, pamoja na vyanzo vingine vya mapato.
Katika hatua nyingine, Ofisi hiyo imeendelea na ubinafsishaji wa viwanda sita vilivyorejeshwa Serikalini ambavyo ni NMC Mzizima, NMC Isaka, CDA Integrated Industry Limited, Kilimanjaro Paddy, Moshi Pesticides na Unique Steel Rolling, ambapo taratibu za kisheria za kukamilisha mchakato huo zinaendelea ili kuhakikisha Serikali inanufaika ipasavyo na mali hizo.
Pia, imefanya uthamini wa mali mbalimbali zilizorejeshwa Serikalini zikiwemo kiwanda cha Tembo Chipboards, mashamba ya maua ya Malalua, Kili Flora Chekereni na USA River Arusha, shamba la Basuto Manyara, mashamba ya NAFCO West Kilimanjaro pamoja na shamba la KPL Mngeta Morogoro, hatua inayolenga kuvutia wawekezaji wenye tija katika maeneo hayo.
Prof. Mkumbo alisema Serikali itaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa uwekezaji wa umma pamoja na mageuzi ya kiutendaji ili kuongeza mchango wa mashirika katika uchumi wa taifa, ukiwemo lengo la kufikia asilimia 8 ya mchango katika Pato la Taifa ifikapo 2050.




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
