` KUTOKA DARASANI HADI UJENZI HALISI: WANAFUNZI WA UDSM WAJIFUNZA CRJE

WANDAMAN HOTEL

KUTOKA DARASANI HADI UJENZI HALISI: WANAFUNZI WA UDSM WAJIFUNZA CRJE

 

Naibu Meneja Mkuu wa CRJE, Zhang Cuishan

Na Mwandishi Wetu - Dar es salaam

Kampuni ya CRJE (East Africa) Ltd imefanya Shindano la kukuza Ujuzi kwa wanafunzi wa Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha  Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM). Shindano hilo lilifanyika kupitia Site Open Day katika mradi mkubwa wa Kampuni hiyo uliopo Mbezi Beach jijini Dar es Salam.

Lengo likiwa ni kuhamisha ujuzi kwa vitendo kutoka Kwa wataalamu wa Kichina kwenda Kwa Wanafunzi wa uhandisi wa Kitanzania ili kuimarisha ushirikiano kati ya China na Tanzania.

Tukio hilo liliwapa wanafunzi kutoka CoET fursa ya kushuhudia ujenzi halisi, usimamizi wa usalama, na utatuzi wa changamoto Katika eneo la ujenzi.

Kupitia ziara ya mradi, na shindano la “Nyota wa Baadaye”, CRJE iliweza kuwaonyesha Wanafunzi wa uhandisi nadharia ya darasani na uhalisia wa kazi hatua ambayo utaweza kutoa mchango mkubwa Kwa CRJE katika kuandaa wataalamu wapya wa uhandisi nchini Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo Bwana Zhang Cuishan, Naibu Meneja Mkuu wa CRJE, amesema kwa muda mrefu China imekuwa na mahusiano mazuri na Tanzania, hivyo wanaona hiyo pia ni fursa katika kuendeleza na kuudumisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili Kwa kuwasaidia wahandisi wanafunzi kupata ujuzi.
Aliongezea kuwa shindano hilo lina maana kubwa kuelekea 2026. “Mwaka 2026 ni miaka 70 ya uhusiano uliotukuka wa kidiplomasia kati ya China na Afrika. Pia ni ‘Mwaka wa Kubadilishana Kati ya Watu wa China na Afrika.’ Hili si shindano la ujuzi tu, bali mazoezi ya kuvuka tamaduni, kuongeza uelewa, na kuimarisha urafiki,” alieleza.

Alitabanaisha: “Ujuzi ndio msingi wa mafanikio, na vipaji ndio nguzo ya maendeleo. Kupitia shindano hili tunajenga daraja la ujuzi. Wafanyakazi wa Kichina na Kitanzania wanashindana, wanajifunza, na kukua pamoja. Ni onyesho la umahiri wa kazi na malengo ya pamoja ya maendeleo.”

CRJE ilianza na ujenzi wa Reli ya Tanzania–Zambia na sasa imekuwepo Tanzania miaka 57. “Tumetekeleza zaidi ya miradi 200 ya ubora. Wajenzi wa Kichina wamehamisha ujuzi, Watanzania wengi wamekuwa wataalamu, na vijana wamejiunga nasi,” alisema Bw. Cuishan. “Madhumuni ya shindano hili ni kuhamasisha roho ya TAZARA, umahiri wa kazi, na bidii — kujifunza kwa kushindana na kuboresha ujuzi kwa vitendo.”

Alisema CRJE inataka vipaji vipya vijitokeze, mawasiliano kati ya wafanyakazi kutoka China na Tanzania waweze kubadilishana ujuzi na teknojia. 

Pia aliomba ushirikiano wa makampuni na vyuo uimarike ili kukuza vipaji vilivyoko vyuoni “Vijana wengi zaidi wajifunze kuhusu CRJE na waje kuchangia maendeleo ya Tanzania,” alisisitiza.

Ujuzi na Usalama Uwandani

Wanafunzi walitembelea maeneo ya kazi na kuona mafundi wa Kichina na Kitanzania wakishirikiana kujenga misingi, kufunga nondo, kumwaga zege, na kupandisha nguzo na sakafu. Waliona pia uendeshaji wa mitambo mizito. Maafisa usalama walieleza matumizi ya PPE na itifaki za kazi. Hivi ni viwango vya CRJE katika kila mradi.
Shindano la “Nyota wa Baadaye” liliwapima washiriki kwa maandishi na vitendo. Walipimwa maarifa ya kiufundi, usimamizi wa miradi, itifaki za usalama na maadili ya kikazi. Majaji walikuwa wahandisi wakuu wa CRJE. Washindi walipata nafasi za intanship na CRJE, zikiunda njia ya moja kwa moja kutoka chuoni kwenda kazini.

Kwa upande wake, Dkt. Innocent Macha, Mkuu wa Chuo Cha CoET, aliishukuru CRJE kwa kusema: “Ushirikiano wenu umeongeza umuhimu kwa kivitendo kwa masomo yetu,” alisema. “Huu ni ushirikiano wa kweli kati ya taaluma na sekta.”

Mwaka jana CRJE na CoET walisaini Makubaliano ili kuweza kuziba pengo kati ya nadhalia ya darasani na vitendo halisia. “Leo naona maono hayo yakitekelezwa. Kujifunza hapa si nadharia bali ni Kwa vitendo,” alibainisha Dkt. Macha.

Aliwaambia wanafunzi: “Hii ni fursa ya kujifunza kwenye mradi halisi, kushirikiana na wataalamu, na kushiriki shindano linalopima maarifa na uwezo wa kufikiri.”

Wanafunzi: “Tumeona Uhalisia”

Martha Chaula, mwanafunzi wa mwaka wa nne Upimaji Wingi, alisema: “Darasani tunakadiria gharama. Hapa nimeona formani wa Kichina na fundi wa Kitanzania wakifanya kazi Kwa pamoja."

Aliongeza: "Tumeweza kujifunza kwa kivitendo yale waliyofundishwa darasani, ukizingatia pia Kampuni ya CRJE wapo mbali katika suala zima la teknolojia, hivyo tumepata kujifunza mambo mapya zaidi."

Zeynat Said, ambaye naye yupo mwaka wa nne chuoni hapo Kwa upande wake alisema kuwa uamuzi wa kampuni hiyo kuwachukuwa wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo, ni heshima kubwa sio tu kwa chuo hicho, bali kwa elimu na maendeleo ya Watanzania kwa ujumla.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464