Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Salum Kitumbo
Na Stella Herman, Shinyanga
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Salum Kitumbo amewahimiza Watanzania kuendelea kuthamini na kuilinda amani iliyopo nchini kwa kutumia vyema muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama msingi wa mshikamano wa kitaifa.
Amesema kuwa umoja huo ni nguzo muhimu
inayochangia utulivu wa nchi na kuleta mshikamano ambao umewezesha taifa kuwa
na utulivu mkubwa ambao unatakiwa kuendelea kulindwa.
Akizungumza wakati wa mahojiano
maalum,Kitumbo amesisitiza kuwa bila kuwepo kwa amani, hakuna shughuli yoyote
ya maendeleo inayoweza kufanyika kwa ufanisi. Ameeleza kuwa mazingira ya
utulivu ndiyo yanayowezesha watu kufanya kazi, kuendesha biashara na kujiletea
maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.
Aidha, amewataka wananchi kutambua
kuwa amani waliyonayo si jambo la bahati mbaya, bali ni matokeo ya juhudi na
misingi imara iliyowekwa na waasisi wa taifa huku akiwakumbusha kuwa ni jukumu
la kila Mtanzania kuilinda na kuidumisha kwa vitendo, ili vizazi vijavyo viweze
kuendelea kufurahia utulivu huo.
Kitumbo amewataja viongozi waasisi
kama Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume kuwa walitoa mchango mkubwa
katika kuijenga Tanzania yenye umoja, mshikamano na amani kwa kuweka msingi wa taifa linalojali utu, haki
na usawa.
Pia alisisitiza kuwa wananchi
wanapaswa kujituma katika kazi na shughuli za uzalishaji, kwani kufanya kazi
kwa bidii ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli, kwani taifa lenye amani lakini
lisilo na juhudi za kiuchumi haliwezi kufikia malengo yake ya maendeleo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464