
Wakulima wa pamba mkoa wa Shinyanga na Simiyu wameeleza kuwa amani ni msingi muhimu unaowawezesha kuendesha shughuli zao za kilimo kwa ufanisi na mafanikio bila kusumbuliwa.
Wamesema bila uwepo wa amani ni
vigumu kwa mkulima kufanya kazi zake kwa utulivu na kupata matokeo chanya,jambo
ambalo linatakiwa kusimamiwa kwa nguvu zote.
Mohamedi Matani mkulima wa pamba
kutoka Mkoa wa Simiyu amesema hali ya utulivu iliyopo kwa sasa imechangia kwa
kiasi kikubwa kuimarika kwa shughuli za kilimo, hususan uzalishaji wa zao la
pamba.
Amesema wanafanya kazi zao kwa bidii wakiamini kuwa
mazingira salama ni kichocheo kikubwa cha maendeleo yao na kuwa na uhakika wa kipato
na chakula kwenye familia.
Said Tangawizi ambaye ni mkulima wa
Shinyanga amesema amani inawawezesha sio
tu kulima bali pia kuvuna na kusafirisha mazao yao bila hofu ya usalama wao
wala mali zao. Hali hiyo imeongeza ari ya uzalishaji na kuimarisha uchumi wa
wakulima .
Katika kusisitiza umuhimu wa amani,
wakulima hao wamekumbushia tukio la Oktoba 29, 2025 wamesema lilisababisha taharuki
na athari kubwa kwa jamii hawatamani kuona wala kusikia tena hali kama hiyo
ikijirudia.
Wamesema tukio hilo linapaswa kuwa
funzo kwa kila Mtanzania juu ya thamani ya amani, wakieleza kuwa ni rahisi
kupotea lakini ni vigumu kurejeshwa,
Pamoja na hayo, wamewataka
watanzania kuendelea kuilinda amani kwa nguvu
zote, wakisisitiza kuwa hakuna mahali pengine pa kwenda kutafuta amani endapo itapotea
ni jukumu la kila mmoja kulinda tunu hiyo muhimu.
Amesema inawawezesha kufanya kilimo na kupata chakula cha uhakika kwani bila chakula cha kutosha, uchumi wa familia na taifa kwa ujumla unaweza kuyumba kwa kiasi kikubwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464