` WATOTO WA MITAANI WALIVYOGUSWA NA UPENDO WA POLISI SHINYANGA

WANDAMAN HOTEL

WATOTO WA MITAANI WALIVYOGUSWA NA UPENDO WA POLISI SHINYANGA

 

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kupitia dawati la jinsia wanawake na watoto, limeadhimisha siku ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu mitaani, kwa kula nao chakula cha pamoja na kuwapatia vifaa vya shule.
Maadhimisho hayo duniani huadhimishwa tarehe 12 kila mwaka, ambapo Jeshi hilo limeadhimisha leo Aprili 10, 2026 katika kituo cha kuwapatia elimu ya maelezi na makuzi watoto hao Nancy Foundation kilichopo Mwalugoye Manispaa ya Shinyanga.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo Janeth Magomi amesema, katika kuadhimisha siku hiyo, wameona ni vyema kukutana na watoto hao ambao huishi mitaani, ili kula nao chakula cha pamoja, kuwapatia vifaa vya shule na elimu ya kupenda kuishi na wazazi au walezi wao ili wapate kutimiziwa mahitaji yao ya msingi.
“Jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia wanawake na watoto, leo tumekuja hapa katika kituo cha Nancy Foundation ili kula chakula cha pamoja na watoto ambao wanaishi mitaani, na kisha kuwapatia vifaa vya shule na elimu ya kupenda kuishi na wazazi wao na siyo kukimbilia mitaani,” amesema Magomi.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Nancy Foundation Ezra Manjerenga, amelishukuru Jeshi hilo kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kwa kupigania haki za watoto hao, na hata kufikia hatua ya kuwakutanisha na wazazi wao.
Amesema, Kituo hicho huwa wanawakutanisha watoto hao kwa kuwapatia chakula na elimu ya malezi na makuzi kwa kuacha kukimbilia mitaani, bali waishi na wazazi wao au walezi, ili wasome shule na kutimiza ndoto zao.

“Baadhi ya watoto hawa wameshafiwa na wazazi wao na wengine hugoma kabisa kurudi kuishi kwa walezi wao, hata ukiwapeleka kesho utawaona mtaani, sisi kama Nancy hua tunawapatia elimu ya kisaikolojia na kuwapatia vifaa vya shule, kuwalipia hela ya chakula na masomo ya ziada na baadhi wameanza kubadilika,” amesema Manjerenga.
Nao baadhi ya watoto hao wakiwamo Linno Omari, wameshukuru kwa chakula hicho na vifaa vya shule, na wengine akiahidi kurudi nyumbani ili kuendelea na masomo.

Wamesema, wamekibilia kuishi mitaani kutokana na kukosa mahitaji mbalimbali nyumbani kwako , kikiwamo chakula sababu wengine wanaishi na bibi zao, na hawana uwezo wa kuwahudumia.

Maadhimisho hayo yana kauli mbiu isemayo” Malezi ya mtoto ni jukumu letu sote.”

MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Picha: Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akigawa chakula kwa watoto wanaoishi mazingira magumu mitaani.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akila chakula cha pamoja na watoto wanaoishi mazingira magumu mitaani.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464