Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Wananchi mkoani Shinyanga, wameeleza kufurahishwa na utaratibu wa usuluhishi wa mashauri ya migogoro mahakamani, wakisema utasaidia kuimarisha mshikamano, kuendeleza undugu na kudumisha amani miongoni mwa jamii.
Wakizungumza leo Aprili 13, 2026 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, kwenye maadhimisho ya wiki ya usuluhishi wa mashauri ya migogoro, wananchi hao wamesema utaratibu huo ni mkombozi kwa pande zinazogombana, ambao unatoa fursa ya kutatua migogoro kwa njia ya maelewano badala ya kuendeleza uhasama.
Mmoja wa wananchi hao Abdala Musa, amesema ana mgogoro wa mirathi, na kwamba yupo tayari kutatuliwa tatizo lao kwa njia ya usuluhishi, ili kutoa haribu mahusiano ya kifamilia.
“Nimefurahishwa na wiki hii ya usuluhishi wa mashauri ya migogoro mahakamani, nipo tayari kukaa na ndugu zangu ambao tuna kesi ya mirathi, ili tulimalize tatizo hili kwa njia ya mazungumzo na tuendelee kuishi kwa amani,” amesema Musa.
Naye Abeli Masanja kutoka wilayani Maswa mkoani Simiyu, ambaye ana kesi ya mgogoro wa ardhi, amesema utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi utapunguza gharama za mara kwa mara za kufika mahakamani kusikilia mashauri, na hata kupoteza muda ambao ungeweza kutumika katika shughuli za kiuchumi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Gadiel Mariki, amesema wiki hiyo ya usuluhishi inalenga kuwafikia wananchi kwa kuwapatia elimu ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo, ikiwa ni pamoja na mashauri yaliyopo mahakamani na yale ambayo hayajafikishwa mahakamani.
Amesema shughuli hizo zimefanyika kuanzia leo Aprili 13 hadi 17, ambapo wameanza na utoaji wa elimu kuhusu usuluhishi na faida zake, na kesho watatoa ya migogoro ya familia na ndoa, Jumatano migogoro ya ardhi, Alhamisi migogoro ya kibiashara na mikataba, na Ijumaa masuala ya usuluhishi yanayohusiana na amani na usalama.
“Elimu hii hutolewa mwisho saa mbili asubuhi, na baada ya hapo tunasajili migogoro iliyopo mahakamani na mipya, kisha kuziita pande zote mbili na kuzungumza nao ili kutafuta suluhu kwa njia ya makubaliano,” amesema Mariki.
Ametaja faida za usuluhishi wa migogoro, kuwa husaidia kupunguza muda wa kushughulikia mashauri mahakamani, hupunguza gharama, na huwawezesha wahusika kumaliza migogoro kwa njia ya amani.
Naye Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya wilaya ya Shinyanga Catherine Langau, amesema usuluhishi wa migogoro unafaida kubwa kwa pande zote mbili na kwamba wakishakubaliana pande zote mbili, makubaliano yao yanaandikwa na kuwa kama hukumu, na kila mmoja ataondoka na nakala ya makubaliano yao.
“lengo kubwa la usuluhishi ni kumaliza mashauri kwa wakati na kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani ,ili kuleta ustawi bora katika jamii, sababu kusikiliza kesi kwa muda mchache watu watapa nafasi ya kufanya shughuli zingine za kiuchumi,” amesema Catherine.
Amesema, kuendesha kesi kwa mfumo wa kawaida wa mahakama unachukua muda mrefu, gharama zinakuwa kubwa, pia unaleta chuki, tofauti na kufanya suluhu ambapo watu wanapatanishwa na kuwa marafiki.
MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Gadiel Mariki akizungumza.
Mwananchi Abdala Mussa akizungumza.