KASHWASA YAKUTANA NA WADAU WA MAJI KUJADILI MPANGO MKAKATI NA MPANGO BIASHARA WA MWAKA 2026-2031
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga Kahama (KASHWASA) wamefanya kikao na wadau na mamlaka za maji ambazo huwauzia maji kutoka Ziwa Victoria, kwa lengo la kuwasilisha na kujadili kwa pamoja mpango mkakati na mpango biashara wa miaka mitano 2026–2031.
Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA, Mhandisi Patrick Nzamba, amesema wamewaita wadau wa maji na mamlaka za maji ambazo huziuzia maji kutoka Ziwa Victoria, kwa ajili ya kujadili mipango ya mamlaka hiyo ya miaka mitano, yenye dhamira ya kuboresha utoaji wa huduma bora ya maji.
“Leo tunajadili mpango mkakati wa Kashwasa wa miaka mitano, na mpango biashara itakayo anza June 2026 hadi 2031, ili kuboresha zaidi utoaji wa huduma bora ya maji, ambapo kwa sasa tunahudumia mikoa sita wilaya 11,” amesema Mhandisi Nzamba.
Amesema, kupitia mpango huo mkakati wamedhamiria kuongeza pia uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 80 kwa siku hadi milioni 120, pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ya mabomba ili kuboresha huduma za maji na kuongeza mtandao.
Ameongeza pia, wamedhamira kupunguza gharama za uendeshaji, hasa kwa upande wa madawa na umeme ambapo wanampango wa kuweka nishati mbadala ya solar, ili kuondokana na utegemezi wa nishati ya umeme pekee, pamoja na kutumia madawa ya bei nafuu kwa ajili ya kutibu maji.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja Jonh Zengo Ngano, akiwasilisha mpango huo mkakati wa miaka mitano, amesema umejumuishwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Ilani ya CCM 2025–2030, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa Awamu ya Sita 2026–2031, na Maendeleo ya Kitaifa SDG na Ajenda ya Umoja wa Mataifa AU 2063.
Amesema, mpango huo wamelenga kuongeza uzalishaji wa maji, kuboresha mazingira ya kijamii na utawala, kupunguza kiwango cha upotevu wa maji kutoka asilimia 17 hadi 14, kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato kwa asilimia 100, kuboresha utoaji wa huduma za maji, na kuboresha miundombinu chakavu ya maji.
Ametaja mipango ya haraka, kuwa ni kupanua kituo cha uzalishaji maji Ihelele, kubadilisha mifumo ya mitambo ya umeme, kubadilisha mita za maji na kuweka za malipo ya kabla, ununuzi wa vifaa vya matengenezo ya mabomba na vifaa vizito, ufungaji wa transfoma za kiotomatiki, kuimarisha usalama wa miundombinu, na kuhifadhi mazingira ya chanzo cha maji.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka KASHWASA, Dk. Edith Kwezi, amewataka wadau kushirikiana kikamilifu na mamlaka hiyo katika mipango yake ya miaka mitano, ili kufikia malengo tarajiwa na kuboresha utoaji wa huduma bora ya maji.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika kikao hicho, Afisa Tarafa wa Oldshinyanga Neema Mkandala, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatirio, amewapongeza KASHWASA kwa mipango yake hiyo, huku akiziagiza mamlaka za maji na vyombo ambavyo vinahudumiwa na KASHWASA, kwamba wawe wanalipa ankara zao za maji kwa wakati, ili watimize wajibu wao wa kutoa huduma bora.
Nao baadhi ya wadau hao akiwamo Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Nzega Ricardo Komanya, wameipongeza KASHWASA kwa kuendelea kujitanua zaidi, na hata kufikisha maji ya Ziwa Victoria wilayani humo, huku akitoa ushauri wa kuimarishwa ulinzi zaidi kwenye vyanzo vya maji.
MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Mgeni rasmi katika kikao hicho Afisa Tarafa wa Oldshinyanga Neema Mkandala akizungumza.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka KASHWASA, Dk. Edith Kwezi akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA, Mhandisi Patrick Nzamba akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja Jonh Zengo Ngano, akiwasilisha mpango mkakati na mpango biashara kutoka KASHWASA.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
