` UWAJIBIKAJI NA ULINZI WA MALI ZA UMMA SI HIARI NI LAZIMA

WANDAMAN HOTEL

UWAJIBIKAJI NA ULINZI WA MALI ZA UMMA SI HIARI NI LAZIMA

 



Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa ulinzi wa mali za umma si jambo la hiari bali ni wajibu wa kisheria na kizalendo kwa kila kiongozi na mwananchi.

Akipokea ripoti za mwaka wa fedha 2024/2025 kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Rais amebainisha kuwa serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa tija.

Alifafanua kuwa uamuzi wa kuwasilisha ripoti ya PPRA kwa mara ya kwanza sambamba na taasisi nyingine unalenga kuongeza uwazi katika sekta ya ununuzi wa umma, ambayo hutumia sehemu kubwa ya kodi za Watanzania, huku akionya kuwa uzembe na ubadhirifu hautafumbiwa macho na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kukiuka maadili ya utumishi.

Ufanisi wa mifumo hiyo umeanza kuonesha matokeo chanya ambapo ripoti ya CAG imebaini kuongezeka kwa kiwango cha hati zinazoridhisha hadi kufikia asilimia 99, huku mashirika ya kibiashara yakifanikiwa kupunguza hasara kwa kiasi kikubwa kulinganisha na miaka ya nyuma.

Aidha, jitihada za makusudi za kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha zimesababisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuvuka malengo ya ukusanyaji kwa kuchangia asilimia 93.1 ya bajeti ya serikali kupitia mapato ya ndani.

Mafanikio haya yanaakisi dhamira ya Rais Samia ya kujenga serikali inayojitegemea na yenye uwezo wa kugharamia miradi yake ya maendeleo kwa kutumia rasilimali zake yenyewe, huku ikizingatia kanuni bora za uandaaji wa hesabu na usimamizi wa mali za umma.

Katika upande wa mapambano dhidi ya hujuma na rushwa, taasisi ya TAKUKURU imefanya kazi kubwa ya uokoaji wa fedha ambapo jumla ya Shilingi bilioni 14.5 zimerejeshwa serikalini kupitia operesheni za uchunguzi na ufuatiliaji wa miradi.

Fedha hizo zinajumuisha limbikizo la ushuru wa huduma kutoka kwa kampuni mbalimbali, urejeshaji wa mikopo ya vyama vya ushirika, na malipo ya gharama za ununuzi wa viwanja vya umma ambavyo awali vilikuwa vimeingia mikononi mwa watu kinyume na utaratibu.

Kiwango hiki cha uokoaji kimeendelea kukua kwa kasi katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa fedha, kikichangiwa na udhibiti wa uhalifu wa kimtandao uliokuwa ukisababisha hasara kubwa kwa benki na wateja kupitia kadi za malipo zilizoghushiwa.

Ili kuhakikisha nidhamu hii inakuwa endelevu, Rais Samia amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyotolewa na taasisi hizo za udhibiti ili kuondoa dosari zinazojirudia kila mwaka.

Moja ya mikakati mipya iliyoelekezwa ni kuanzishwa kwa "Orodha ya Fedheha" (Name of Shame) kupitia PPRA, itakayotaja hadharani taasisi zinazofanya vibaya katika usimamizi wa ununuzi kuanzia mwaka ujao. Hatua hizi, zikiambatana na agizo kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kukusanya madeni ya michango ya wafanyakazi yenye thamani ya matrilioni ya shilingi, zinadhihirisha kuwa serikali imepania kujenga utamaduni wa uadilifu utakaolinda rasilimali za taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464