Tanzania imeendelea kung’ara katika ulingo wa kifedha duniani, baada ya kushinda tuzo ya kimataifa ya fedha za miundombinu mwaka 2026, kutokana na ubunifu na umakini wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kusimamia mikataba mikubwa ya kimaendeleo.
Ushindi huu umetokana na mafanikio ya kupatikana kwa mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani bilioni 1.78 kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Umeme (SGR) kipande cha tatu na nne.
Tuzo hiyo ilipokelewa jijini Cape Town, Afrika Kusini na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bwana Rished Bade, ikihusisha utambuzi wa taasisi za kimataifa za benki na masoko kwa nchi zinazofanya vizuri katika kuingia mikataba bora ya kifedha kupitia masoko ya mitaji na mikopo.
Utafutaji wa ufadhili wa mradi huo wa kimkakati umekuwa kielelezo cha diplomasia ya uchumi, ambapo Tanzania imefanikiwa kuunganisha taasisi za bima kutoka nchi za Sweden, Poland, na Italia, pamoja na benki za maendeleo za kikanda kwa uratibu wa Benki ya Standard Chartered.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, na Katibu Mkuu Dk. Natu Mwamba wameeleza kuwa ushindi huu ni matokeo ya moja kwa moja ya maelekezo na uongozi thabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan katika usimamizi wa deni la serikali. Mafanikio haya yanaiweka Tanzania katika nafasi nzuri kwenye masoko ya fedha duniani, yakionyesha uwezo wa nchi kubuni miundo ya kifedha inayovutia uwekezaji wa nje huku ikizingatia maslahi ya taifa.
Vigezo vilivyotumika kuipatia Tanzania tuzo hiyo ni pamoja na ubunifu wa muundo wa kifedha, unafuu wa masharti ya mikataba, na ubora wa utekelezaji wa mipango ya ufadhili wa miradi. Hii inadhihirisha kuwa serikali si tu inatekeleza miradi mikubwa ya miundombinu, bali inafanya hivyo kwa weledi wa hali ya juu unaozingatia uendelevu wa deni na tija kwa uchumi wa nchi na Ukanda wa Maziwa Makuu.
Tuzo hizi, ambazo zimekuwa zikitolewa tangu mwaka 2014, zinalenga kuzitambua nchi zinazotumia soko la mitaji kwa ufanisi mkubwa katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Ushindi huu wa miundombinu umekuja wakati muafaka, kwani hivi karibuni Tanzania pia imetwaa ushindi wa jumla wa mwaka katika tuzo za Jumuiya ya Madola kuhusu usimamizi wa deni la umma zilizotangazwa jijini London.
Aidha, nchi imenyakua Tuzo ya Ofisi Bora Kanda ya Afrika kupitia Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali ndani ya Wizara ya Fedha, hali inayothibitisha kuwa mifumo ya ndani ya udhibiti na usimamizi wa fedha imeimarika.
Mfululizo wa tuzo hizi za kimataifa ni kielelezo tosha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inajenga msingi imara wa kuaminika kimataifa, jambo linalochochea kasi ya maendeleo na ustawi wa Watanzania kupitia miradi ya kimkakati.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464