` MKAKATI WA MAKAA YA MAWE: SERIKALI YALENGA MAGEUZI YA VIWANDA NA NISHATI

WANDAMAN HOTEL

MKAKATI WA MAKAA YA MAWE: SERIKALI YALENGA MAGEUZI YA VIWANDA NA NISHATI

 


Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa makaa ya mawe ni rasilimali ya kimkakati itakayotumika kama mhimili mkuu wa mageuzi ya uchumi wa viwanda na kuongeza thamani ya malighafi nchini.

Akizungumza Machi 30, 2026, jijini Dodoma katika kikao na wadau wa sekta hiyo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amebainisha kuwa nchi imejaliwa utajiri wa kutosha wa nishati hiyo, hivyo ni lazima itumike kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Waziri Mavunde ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo ya dhati kuhakikisha rasilimali za taifa zinachangia moja kwa moja katika maendeleo ya nchi, huku akiahidi kufanya maboresho ya kanuni na taratibu ili kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara.

Katika kikao hicho, wadau wameibua changamoto nzito zinazokwamisha ushindani wa makaa ya mawe ya Tanzania katika soko la kimataifa, hususan dhidi ya nchi za Msumbiji na Afrika Kusini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tancoal, Daniel Mukenzi, amebainisha kuwa gharama kubwa za uzalishaji, mirabaha inayotozwa kwa Dola za Marekani, na ongezeko la gharama za upakiaji katika Bandari ya Mtwara ni vikwazo vikubwa vinavyopandisha bei ya bidhaa hiyo.

Wadau wameiomba serikali kupitia upya mfumo wa bei elekezi uwe shirikishi zaidi ili kuleta uhalisia wa gharama za uchimbaji, pamoja na kudhibiti wafanyabiashara wa nje wanaonunua nishati hiyo na kwenda kuiuza kwa bei ya chini inayodhoofisha soko la ndani.

Ili kuimarisha umoja na utatuzi wa changamoto hizo, Waziri Mavunde amewahimiza wadau wa makaa ya mawe kuanzisha chama rasmi kitakachowaunganisha na kurahisisha mawasiliano na serikali.

Aidha, ametoa onyo kali dhidi ya vitendo vya baadhi ya wafanyabiashara kuuza nishati hiyo kwa bei ya chini isiyo halali, akisisitiza kuwa mabadiliko yoyote ya kanuni yatakayofanywa lazima yazingatie maslahi mapana ya taifa na kulinda soko. Serikali imeahidi kufanyia kazi malalamiko ya gharama za usafirishaji na kodi ili kuhakikisha wazalishaji wa ndani wanapata tija na uwezo wa kushindana katika soko la Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Katika hatua inayoonyesha matokeo ya awali ya mkakati huo, kampuni ya A1 Steels Tanzania LTD imetangaza mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha chuma jijini Dodoma kitakachotumia takribani tani 20,000 za makaa ya mawe kwa mwaka. Mradi huu unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ajira na kielelezo cha namna rasilimali za madini zinavyoweza kuongeza thamani ya uzalishaji wa ndani.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464