` TANZANIA YAZIDI KUNG'ARA KIMATAIFA: KUTEULIWA KITUO CHA MAFUNZO YA MAZINGIRA NI JIBU KWA WACHOCHEZI

WANDAMAN HOTEL

TANZANIA YAZIDI KUNG'ARA KIMATAIFA: KUTEULIWA KITUO CHA MAFUNZO YA MAZINGIRA NI JIBU KWA WACHOCHEZI

Hatua ya Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali ya Umoja wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi kuiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa kituo cha mafunzo ya vijana kuhusu mazingira ni kielelezo tosha kuwa nchi yetu inazidi kuaminika na kukubalika katika jumuiya ya kimataifa.

Teuzi hii iliyofanyika katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi huko Addis Ababa, Ethiopia, inadhihirisha kuwa juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika diplomasia na hifadhi ya mazingira zimezaa matunda yanayoonekana.

Wakati baadhi ya watu wakijaribu kupiga kampeni za kuitenga Tanzania na kueneza maneno ya uchochezi, jumuiya ya kimataifa imeendelea kuipa nchi heshima ya kipekee, ikionyesha kuwa kelele hizo hazina nguvu ya kuzuia kasi ya maendeleo ya taifa letu.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amebainisha kuwa kuteuliwa kwa Tanzania kama mjumbe wa kudumu na mwenyeji wa kituo hicho kutafungua milango ya fursa adhimu kwa vijana wa Kitanzania.

Kituo hicho kitakachotoa mafunzo kuhusu mabadiliko ya tabianchi na mazingira, kitawasaidia vijana kupanua wigo wa ushiriki wao katika mijadala ya kimataifa na kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazoibuka katika sekta hiyo. 

Hatua hii ni dongo la moto kwa wale wanaodai kuwa nchi imepoteza dira, kwani ukweli unathibitisha kuwa Tanzania sasa ni kimbilio la masuala ya kitaalamu na kimkakati barani Afrika, jambo linalojenga taswira chanya na imara ya nchi yetu duniani.
Juhudi hizi za serikali zinaungwa mkono kwa dhati na wadau mbalimbali wakiwemo wasanii na taasisi zisizo za kiserikali, kama inavyothibitishwa na Balozi wa Mazingira wa UNEP, Bi. Frida Amani, aliyewahimiza vijana kuungana na serikali kutunza mazingira kama fursa ya kiuchumi.

Kadhalika, taasisi ya The Green Samia imekuwa mstari wa mbele katika kampeni za usafi na upandaji miti, ikionyesha mshikamano uliopo kati ya jamii na uongozi wa nchi.

 Ushirikiano huu wa pamoja ndio injini inayoiwezesha Tanzania kusonga mbele kwa ujasiri, ikipuuza migogoro ya kutengenezwa na badala yake ikijikita katika kutatua changamoto za kidunia kama mabadiliko ya tabianchi.

Kuzinduliwa kwa kituo hiki jijini Dar es Salaam kunathibitisha kuwa Tanzania si nchi ya kutengwa, bali ni nchi kiongozi inayotengeneza suluhu kwa matatizo ya vijana wa Afrika.

Ni dhahiri kuwa wale wanaofanya kampeni za kuichafua nchi wamezidi kupoteza dira, kwani takwimu na matukio ya kidiplomasia yanathibitisha kuwa Tanzania inazidi kupendwa, kuheshimiwa, na kuaminiwa kuliko wakati mwingine wowote.

 Taifa linaendelea kujenga ustawi wake kwa vitendo, likiamini kuwa umoja na mshikamano wa ndani ndio kinga dhidi ya chuki yoyote inayolenga kudhoofisha nafasi yetu katika meza ya mataifa makuu duniani.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464